DAR ES SALAAM; MWAKA 2025 utaendelea kukumbukwa kama kipindi cha kihistoria kilicholeta mageuzi makubwa katika sekta ya usafirishaji na miundombinu nchini Tanzania.

Katika mwaka huu, serikali iliongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati iliyolenga kuboresha usafiri wa watu na mizigo, kuchochea uchumi, na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha usafirishaji kikanda.

Miradi hiyo ni pamoja na Reli ya Kisasa (SGR), Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Daraja la Kigongo–Busisi na Bandari Kavu ya Kwala.

Reli ya Kisasa (SGR): Enzi Mpya ya Usafirishaji wa Mizigo

Juni 27, 2025, Tanzania iliandika historia nyingine baada ya kuzindua rasmi safari ya treni ya mizigo kati ya Dar es Salaam na Dodoma kupitia reli ya kisasa ya SGR.

Hatua hii ilifungua ukurasa mpya wa usafirishaji mzito wa bidhaa, ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi kuanza rasmi huduma hiyo kwa kutumia reli ya kisasa.

Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26, Serikali ilitenga Shilingi trilioni 1.51 kwa ajili ya utekelezaji wa vipande mbalimbali vya mradi wa SGR.

Uzinduzi wa treni ya mizigo ulifanyika baada ya majaribio ya kina na ukaguzi wa vyombo vya usalama, ukifuatia mafanikio ya huduma ya abiria iliyovutia zaidi ya wasafiri milioni 2.5 tangu ilipoanza Juni 2024.

Kwa uwezo wa kubeba tani 10,000 kwa safari moja ambayo sawa na malori 500, treni ya mizigo ya SGR inatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa barabara, gharama za usafirishaji, na kuongeza ufanisi wa biashara za ndani na za kuvuka mipaka.

Mabasi Yaendayo Haraka (BRT): Mbagala wafaidi mwendokasi

Mwaka 2025 pia uliashiria mapinduzi makubwa katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), hususan katika Awamu ya Pili. Serikali ilitumia Shilingi bilioni 285.1 kujenga kilometa 20.3 kati ya Gerezani na Mbagala Rangi Tatu, hatua iliyopanua mtandao wa usafiri wa umma jijini Dar es Salaam.

Mwezi Agosti 2025, mabasi 99 ya BRT yaliwasili nchini ili kuanza kutoa huduma na kupunguza changamoto za usafiri kwa wakazi wa jiji. Agosti 13, 2025, Waziri Mkuu wa wakati huo, Kassim Majaliwa alikagua mabasi hayo pamoja na miundombinu muhimu ikiwemo vituo vya Gerezani na Mbagala Rangi Tatu, huku akisisitiza umuhimu wa kuboresha usafiri wa umma kama kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi.

Katika ukaguzi huo, alitembelea pia kituo maalumu cha kujazia gesi kwa mabasi hayo kilichojengwa Mbagala Rangi Tatu, na kutoa maelekezo kwa waendeshaji kuhakikisha kazi zinafanyika usiku na mchana ili kukamilisha maeneo yote yaliyobaki. Hatua hiyo iliwezesha mradi kuanza kutoa huduma kikamilifu.

Mabasi ya mwendokasi kutoka Mbagala yakaanza Oktoba 12, 2025 lakini yalisitishwa siku chache baadaye kwa baadhi ya mabasi yake kuhamishiwa njia ya Kimara, kabla ya mradi huo kurejea rasmi Novemba 20, 2025.

Daraja la JP Magufuli lazinduliwa rasmi

Daraja la Kigongo–Busisi (Daraja la JP Magufuli), lililozinduliwa Juni 2025, limekuwa nguzo muhimu ya kuunganisha mkoa wa Mwanza na mikoa jirani pamoja na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Daraja hilo lenye urefu wa kilometa 3 limegharimu Shilingi bilioni 718, na limepunguza muda wa kuvuka Ziwa Victoria kutoka zaidi ya saa mbili ukichanganya na muda wa kusubiri kwa kutumia vivuko hadi dakika chache tu.

Matokeo yake ni kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria kwa wakazi wa Mwanza, Geita, Kagera na nchi jirani. Ujenzi wa daraja hilo ulianza Februari 2020 na kukamilika rasmi Juni 2025.

Bandari Kavu ya Kwala: Kituo kipya cha biashara na usafirishaji

Julai 31, 2025, Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, alizindua rasmi Bandari Kavu ya Kwala, mradi uliolenga kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kuboresha mtiririko wa bidhaa.

Uzinduzi huo uliambatana na kuanza kwa huduma ya treni ya mizigo ya SGR kuelekea Kwala, mapokezi ya mabehewa mapya 50 ya reli ya zamani (MGR) pamoja na 20 yaliyokarabatiwa, na uwekaji wa jiwe la msingi katika Kongani ya Viwanda ya Kwala.

Bandari Kavu ya Kwala ina uwezo wa kuhudumia makasha 300,000 kwa mwaka, hatua inayotarajiwa kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya asilimia 30 na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa.

Kwa ujumla, mwaka 2025 umeweka alama isiyofutika katika historia ya maendeleo ya miundombinu nchini Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *