Dar es Salaam. Katikati ya sintofahamu kuhusu kuondolewa kwa kamera za CCTV katika barabara za Goba Center na Goba Njia Nne wilayani Ubungo, kukihusishwa na vurugu zilizotokea Oktoba 29 mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amefunguka na kueleza chanzo cha hali hiyo.

Kamera hizo za CCTV ziliwekwa katika maeneo hayo Juni mwaka huu, kwa lengo la kufuatilia na kudhibiti mwenendo wa magari, kupunguza ukiukwaji wa sheria za barabarani, na kupunguza msongamano wa magari katika barabara hizo.

Mpango huo, ulioandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ulikuwa na lengo la kuimarisha nidhamu miongoni mwa madereva, kurahisisha usimamizi barabarani, na kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara.

Hata hivyo, katika eneo la Goba Center na Goba Njia Nne, imebainika kamera za CCTV zimeondolewa ndani ya miezi miwili iliyopita.

Hali hiyo imeibua sintofahamu miongoni mwa wananchi, huku baadhi yao wakihoji mitandaoni sababu za kuondolewa kwa kamera hizo katika kipindi hicho.

Wengine walitaka kufahamu matukio yoyote yaliyoripotiwa kabla ya kuondolewa kwa kamera hizo, ambazo ziliondolewa muda mfupi tu baada ya vurugu za Oktoba 29.

Baadhi ya wananchi pia walisema wanataka kujua endapo malengo ya awali ya ufungwaji wa kamera hizo yamekamilika kabla ya kuondolewa, huku wengine wakidai kamera hizo zilikuwa zimenasa matukio mengi ya vurugu za Oktoba 29 yakiwemo mauaji, na hivyo kuhoji iwapo kuondolewa kwake kulifanyika kwa makusudi na kwa ushawishi wa wahusika fulani.

Akizungumza na Mwananchi leo, Desemba 30, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando amefafanua sababu za kutokuwepo kwa kamera hizo, akibainisha kuwa ziling’olewa na baadhi ya waandamanaji wakati wa vurugu zilizotokea Oktoba 29.

“Ziling’olewa na watu waliofanya maandamano wakati wa vurugu za Oktoba 29, wale wanaosema ziling’olewa na polisi, si kweli wanapotosha.

“Hakuna polisi wala hakukuwa na sababu zozote za polisi kung’oa kamera zile, kwa kuwa hata sisi tungezitumia kujua nani alihusika kwenye vurugu.

“Sasa unang’oaje kitu ambacho kingekusaidia kukupa ushahidi wa waliohusika kwenye zile vurugu katika eneo hilo? Kama nilivyosema hakukuwa na sababu ya polisi kuzing’oa, ziliondolewa na waandamanaji,” amesema Msando.

Alipoulizwa kama kuna mpango wa kufunga kamera nyingine kuendeleza jitihada za Wilaya ya Ubungo za kuimarisha nidhamu miongoni mwa madereva, kurahisisha usimamizi wa trafiki, na kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara, Msando amesema upo na unaendelea kuandaliwa.

“Kwa sasa huo ni mpango wa Serikali, zile za Goba awali niliweka mimi kama Msando kwa gharama zangu, lakini sasa Serikali ina mpango wa kuweka kamera kwenye maeneo yote muhimu ya barabara nchini kama ilivyofanyika Dodoma.

“Mpango huo utafanyika pia kwenye maeneo mengine ya nchi, hivyo ni mpango wa Serikali kwa maeneo yote muhimu ya nchi yetu, kama ilivyofanyika Dodoma,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *