
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameunda tume ya kupitia na kutathmini masuala ya fidia yanayotokana na utekelezaji wa miradi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Unguja na Pemba.
Hatua hiyo inakuja kufuatia kuibuka kwa malalamiko ya wananchi katika maeneo yanakotekelezwa miradi hiyo ya maendeleo, wakidai kulipwa fedha ndogo isiyoendana na thamani ya mali zao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano Desemba 31, 2025 na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Raqey Mohamed, Rais Mwinyi ameteua tume ya wataalamu wanane kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi kufanya kazi hiyo.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikutaja muda ambao tume hiyo itachukua kukamilisha majukumu yake.
Wajumbe wa tume hiyo ni Salum Othman Simba ambaye ni mstaafu na mtaalamu wa masuala ya uthamini, Mussa Kombo Mrisho (mwanasheria kutoka Ofisi ya Rais Ikulu), Khamis Muhidini Bakari (mhandisi kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege) na Fauzia Sindi Hassan (Msajili wa Bodi ya Usajili ya Makandarasi).
Wengine ni Sabrina Yussuf Hassan ambaye ni mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Mwanaidi Suleiman Ali (mtaalamu wa masuala ya jamii) kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca), Ramadhani Nassoro Mwinyi (mtaalamu wa fedha) kutoka sekta binafsi na Mzee Abdallah Khatib (mtaalamu wa umma) kutoka sekta binafsi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, wananchi wanaombwa kutoa ushirikiano kwa tume hiyo itakapofika katika maeneo husika, kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake.
Wakizungumza kuhusu kuundwa kwa tume hiyo, baadhi ya wananchi wa Kwerekwe wamesema wana matumaini kuwa itatoa suluhu ya kudumu.
“Tathmini inayofanywa inachanganya, wengine wanalipwa fedha nyingi na wengine wanapunjwa. Tunaamini tume hii itakuja na majibu mazuri, tunapongeza hatua hii,” amesema Rajab Hassan.
Hata hivyo, kuundwa kwa tume hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa Dk Mwinyi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, alipokutana na makundi mbalimbali ya wananchi.
Moja ya kero iliyowasilishwa na wananchi kwake, ilikuwa madai ya kudhulumiwa malipo ya fidia.
Kero hiyo ilijitokeza zaidi katika maeneo ya Fumba, Nyamanzia na Dimani, ambako wananchi wengi waliopata fursa ya kuzungumza kwenye mikutano ya kampeni.
Wakati akijibu hoja hizo, Dk Mwinyi alikiri kuwepo kwa changamoto katika baadhi ya tathmini na kuwaahidi wananchi kuunda tume maalumu endapo angerudi madarakani.
Hata hivyo, Rais Mwinyi aliwahi kufafanua kuwa, wakati mwingine baadhi ya wananchi huendeleza maeneo yasiyoruhusiwa kisheria, hali inayosababisha gharama za fidia kuwa kubwa kuliko gharama za mradi wenyewe.
“Wananchi ni muhimu kwa maendeleo, lakini pia miradi lazima itekelezwe kwa sababu bila miradi hatuwezi kupiga hatua za maendeleo,” alisema Dk Mwinyi.
Malalamiko ya fidia pia yaliibuka katika mradi wa ujenzi wa barabara za mjini unaohusisha madaraja mawili ya juu ya Amani na Kwerekwe, baadhi ya wananchi walilalamikia fidia ndogo na kutishia kugoma kuondoka katika maeneo yao.
Hatua hiyo iliwalazimu mawaziri wawili wa wakati huo, akiwamo wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Khalid Mohamed Salum, kukutana na wananchi hao katika ukumbi wa Kwa Wazee.
Katika mkutano huo, mawaziri waliwaeleza wananchi mpango wa Serikali wa kufanya tathmini upya ili kupata uhalisia wa fidia stahiki kwa kila mhusika.
Kwa mujibu wa maelezo ya Dk Mkuya, tathmini ya awali haikuhusisha thamani ya ardhi, jambo lililosababisha baadhi ya wananchi kulipwa fidia ndogo.
Baadaye, Dk Mwinyi alisema Serikali iliamua kutafuta kampuni binafsi kufanya tathmini mpya baada ya kubaini changamoto kwa mthamini wa Serikali.