MABOSI wa Dodoma Jiji wameanza maboresho ya kikosi hicho kimya kimya katika dirisha hili dogo linalofunguliwa rasmi leo Januari 1, 2026, ambapo kwa sasa wanakaribia kupata saini ya mshambuliaji nyota raia wa DR Congo, Osako Ngeleda Modeste.

Chanzo kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti, Modeste amefikia makubaliano ya kujiunga na kikosi hicho, ambapo muda wowote kuanzia sasa atatua Tanzania kwa ajili ya kusaini mkataba wa miaka miwili aliowekewa mezani.

“Kilichobakia ni kusaini tu mkataba ila makubaliano ya pande mbili yamefikiwa, ni mchezaji aliyecheza timu kubwa ambazo tunaamini ana uzoefu pia wa kutosha na atakuwa ingizo sahihi katika eneo letu la ushambuliaji,” kilisema chanzo hicho.

Mtoa taarifa huyo amesema miongoni mwa mapendekezo ya benchi la ufundi la kikosi hicho kinachofundishwa na Kocha, Amani Josiah, ni kuongezewa mshambuliaji atakayeongeza ushindani, ambapo kwa Modeste wanaona ni mtu sahihi katika eneo hilo.

Modeste ni nyota aliyecheza timu za AS Vita Club ya DR Congo, Cape Town Spurs ya Afrika Kusini, Clube Recreativo Desportivo do Libolo, Grupo Desportivo Interclube, Atletico Sport Aviacao na Santa Rita de Cassia za Angola.

Dodoma Jiji inasaka mshambuliaji ili kuongeza nguvu eneo hilo, kwani hadi sasa timu hiyo imecheza mechi nane za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo washambuliaji wote wa kikosi hicho wamefunga mabao manne tu, jambo linalowaingiza tena sokoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *