Katika kambi ya muda ya wakimbizi ya Busuma Mashariki mwa Burundi kwenye jimbo la Ruyigi wakimbizi ni wengi wakiishi kwenye mahema yaliyojengwa kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Maaifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Maseka aliyelazimika kufungasha virago na watoto wake ni miongoni mwa maelfu ya wakimbizi hawa. Anasema sasa wako salama hawahofii tena kifo kwa mtutu wa bundiki lakini usalama pekee hautoshi kwani chakula ni haba dawa ni chache na huduma kwa watoto wao wagonjwa zimeelemewa. 

Tulikimbia tumetoka mbali, na hatukuwa hata na kitu kimoja. Ndio Mungu akatusaidia wakatufungulia mpaka tukaingia hapa Burundi na hapa sasa tuko wapita njia  tunazunguka na tunasumbuka sana tunasumbuka. 

Anaongeza kuwa kila siku, foleni ni ndefu ya kupata huduma huku familia zikisubiri msaada kwa saa nyingi, bila uhakika wa kupata chochote wanachohitaji.

“Njaa inatupiga tuno nje kwenye foleni tukilowana, watoto wote ni wagonjwa. Kila siku, watoto, ni mahoma, mafua, kikohozi. Sasa hapa tunasumbuka wanatuambia watatuletea dawa lakini tunaenda kuuziwa na pesa hatuna. Unaenda asubuhi saa moja na itafika saa kumi bila kupata dawa.” 

Kwa mujibu wa UNHCR changamoto hizi ndio uhalisia wa zaidi ya wakimbizi 88,000 wa Congo ambao wamesaka usalama nchini Burundi kwa sasa. 

UNHCR inaonya kuwa mahitaji ni makubwa kupita uwezo, na rasilimali zilizopo zimeelemewa na mahitaji lukuki. Kwa Maseka wanachokiomba si kingine bali mahitaji ya msingi tu kwani

“Tunasumbuka tunaona na wanatuambia watatuletea chakula, chakula wanapika lakini hatukioni chakula hakitufikii hapo sababu watu ni wengi walianza kupika na kugawa hicho chakula unajikuta huna hata chakula”

Licha ya hali hiyo, familia zaidi zinaendelea kuwasili, zikikimbia ukosefu wa usalama na ghasia zinazoendelea nyumbani Mashariki mwa Congo. 

Mashirika ya kibinadamu likiwemo la UNHCR yanasema ufadhili na msaada wa haraka ni muhimu ili kutoa mahitaji ya msingi kama chakula, huduma za afya, makazi na ulinzi na kuzuia mgogoro wa kibinadamu kuwa mbayá zaidi.

UNHCR inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua sasa ili kuokoa maisha na kurejesha utu kwa familia kama ya Maseka, ambazo tayari zimepoteza kila kitu wakiwemo ndugu na jamaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *