
Siku 90 zilizobainishwa na Katiba kwa ajili ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu, unakaribia kumalizika.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna dalili za wazi kuwa mchakato huo uko mbioni kukamilika, hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na msimamo wa Chama cha ACT – Wazalendo, ambacho ndicho kinachotarajiwa kuungana na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuunda SUK.
Kwa mujibu wa ACT – Wazalendo, chama hicho hakiwezi kushiriki katika kuunda SUK kwa sababu kinahoji uhalali wa uongozi uliopo, kikidai uchaguzi haukuzingatia misingi ya kuwa huru na wa haki.
Katika orodha ndefu ya sababu walizozitoa, ACT – Wazalendo inadai uchaguzi ulijaa dosari kubwa, ikiwamo madai ya watu kupiga kura zaidi ya mara moja au hata mara tatu, wakiwamo watoto walio chini ya umri wa miaka 15 pamoja na makarani wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa chama hicho, demokrasia ya kweli inahitaji uongozi wenye ridhaa ya wananchi, lakini hali hiyo haikujitokeza katika uchaguzi wa siku mbili uliofanyika Zanzibar.
Badala yake, chama hicho kinadai kulikuwapo kwa uchafuzi wa mchakato wa uchaguzi uliokiuka Katiba, sheria na kanuni za uchaguzi.
Aidha, kinadai hakukuwa na uwazi katika uhesabuji wa kura wala katika kutangaza matokeo.
ACT – Wazalendo pia kinadai kuwa CCM haikushinda hata jimbo moja katika Kisiwa cha Pemba na inaona ni jambo la kushangaza na lisiloelezeka kwa wao kukosa ushindi katika uchaguzi wa udiwani, uwakilishi na ubunge, wakisema matokeo hayo hayaingii akilini kwa hali halisi ya kisiasa ya eneo hilo.
Kutokana na hali hiyo, ACT – Wazalendo imefungua kesi mahakamani kupinga na kudai kutenguliwa kwa matokeo ya majimbo 20, ambapo kesi hizo zimeanza kusikilizwa katika Mahakama za Unguja na Pemba.
Hata hivyo, ni vigumu kutabiri ni lini kesi hizo zitafikia tamati. Uzoefu wa chaguzi zilizopita unaonesha kesi za uchaguzi huwa zinasuasua kwa muda mrefu, mara nyingine hadi uchaguzi mwingine unapokaribia, au hata kutotolewa kabisa kwa uamuzi wala maelezo ya kina.
Wakati wananchi wakisubiri matokeo ya kesi hizo, bado hakuna dalili ya kuwepo kwa maelewano ya kisiasa.
Kwa mtazamo wa ACT – Wazalendo, SUK miaka yote ipo kwa jina tu bila utekelezaji wa dhati katika utendaji kazi.
Swali kubwa linaloibuka ni nini kitatokea baada ya kumalizika kwa siku 90 mwishoni mwa Januari, suala ambalo limebaki kuwa fumbo gumu kulitafsiri.
Hii ni kwa sababu vyama vingine vyote vilivyoshiriki uchaguzi havikufikia vigezo vya kushiriki katika SUK kutokana na kupata kura chache.
Hakuna hata chama kimoja, mbali na CCM na ACT – Wazalendo kilichopata zaidi ya nusu asilimia ya kura katika matokeo ya majimbo wala katika uchaguzi wa Rais wa Unguja na Pemba.
Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Serikali, CCM wala ACT -Wazalendo inayoeleza kinachoendelea au iwapo kuna mazungumzo yoyote yanayoendelea kwa lengo la kufikia maridhiano.
Hata hivyo, zipo fununu zinazoashiria kuwapo kwa juhudi zisizo rasmi za kujaribu kupata suluhu. Pamoja na hilo, ACT – Wazalendo inadaiwa kuwa imekaza msimamo wake, ikisema haiwezi hata kufikiria kushiriki maridhiano kwa sababu uchaguzi ulikuwa na mizengwe isiyovumilika na kwamba, wenzao hawana uaminifu na hujisahau viapo wanavyokula mara wapatapo madaraka.
Na Wakati Zanzibar ikiadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi, bado kuna hilo wingu zito la hali ya kisiasa juu ya visiwa hivyo.
Kutoelewana kati ya vyama hivi viwili vyenye mvuto mkubwa wa kisiasa, bado hakujulikani kama kutasababisha mvua kubwa, rasha rasha ndogo au hatimaye wingu hilo litatoweka bila madhara na mwelekeo wake ukabaki kuwa kitendawili.
Huu ni mtihani mwingine mkubwa wa kisiasa kwa Zanzibar tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, lakini unaweza kusemwa kuwa una utata na mzigo mkubwa wa sintofahamu kuliko mitihani yote iliyotangulia.
Katika nyakati zilizopita, viongozi wastaafu wa Zanzibar, Muungano na wa dini, waliwahi kuchukua nafasi ya kusaidia kufanikisha muafaka wa kisiasa.
Safari hii, ACT – Wazalendo inaonekana kukosa imani na makundi hayo, ikidai kuwa juhudi hizo hufanywa si kwa nia njema bali kwa lengo la kufunika maovu yaliyotendeka, badala ya kuzingatia maslahi ya Zanzibar na wananchi wake.
Kwa sasa, macho na masikio yanaelekezwa mahakamani kusubiri yatakayojiri. Hata hivyo, hali ilivyo sasa ni kama ngoma nzito inayoendelea kupigwa bila hata wapigaji wake kujua ni miziki ipi itakayozalisha maelewano yenye tija kwa Zanzibar na Muungano kwa ujumla.