Unguja. Tatizo la masafa marefu yaliyokuwa yakiwakabili madaktari na wahudumu wa afya katika utoaji wa huduma Hospitali ya Wilaya ya Kitogani limepata ufumbuzi baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga nyumba za makazi karibu na hospitali hiyo.
Hatua hiyo inatarajiwa kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi, hususan wagonjwa wa dharura, kwa kuwa wataalamu wataweza kupatikana muda wote bila kusubiriwa kutoka maeneo ya mbali.
Ufunguzi wa nyumba hizo umefanyika leo Desemba 31, 2025, ambapo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, alizindua rasmi makazi hayo ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akitoa taarifa ya kitaalamu mbele ya Rais, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Mgereza Miraji Mzee, amesema baada ya kufunguliwa kwa hospitali hiyo, Serikali iliona umuhimu wa kujenga makazi ya wafanyakazi karibu na hospitali ili kupunguza changamoto za usafiri na kuimarisha huduma za afya.
“Hatua hii itaipunguzia Serikali gharama kubwa za usafiri wa kuwafuata madaktari, hususan wakati wa usiku na siku za mapumziko panapotokea dharura,” amesema Dk Mgereza.
Amesema mradi huo ulianza Januari 2024 na kukamilika Septemba 2025, ukichukua miezi 20 kwa gharama ya Sh5.5 bilioni zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa Dk Mgereza, ujenzi huo umefanywa na mkandarasi Quality Building Contractor, ambaye tayari amelipwa Sh5.4 bilioni sawa na asilimia 97.5 ya thamani ya mkataba, huku usimamizi ukifanywa na mshauri elekezi, Mecco.
Mradi huo umehusisha ujenzi wa jengo moja la ghorofa tatu (G+3) lenye uwezo wa kuhudumia familia 16, ambapo wanane wataishi kwenye nyumba za vyumba vitatu na wanane kwenye nyumba za vyumba viwili, likiwa limewekewa huduma zote za msingi.
Amesema kukamilika kwa nyumba hizo ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya Wilaya ya Kusini na Kati, pamoja na kutoa uhakika wa makazi kwa madaktari bingwa na wataalamu wabobezi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Mwinyi ameiagiza Wizara ya Afya kuanzia sasa kushirikisha Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), katika ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa sekta ya afya.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza wakati akizindua nyumba za wafanyakazi katika hospitali ya Wilaya ya Kitogani Mkoa wa Kusini Unguja
Amesema ZHC lina uzoefu na uwezo mkubwa wa kusimamia miradi ya ujenzi kwa ufanisi na kwa gharama nafuu zaidi.
“Jengo hili limechukua miezi 20 kukamilika, wakati lingeweza kujengwa ndani ya miezi sita kama lingeendeshwa na ZHC,” amesema Rais Mwinyi.
Ameongeza kuwa gharama za ujenzi zilikuwa kubwa ikilinganishwa na zile zinazotumiwa na ZHC, ambalo hujenga na kuuza nyumba kwa gharama kati ya Sh130 milioni hadi Sh150 milioni huku likipata faida.
Rais Mwinyi amesisitiza kuwa Wizara ya Afya inapaswa kujikita katika jukumu lake la msingi la ujenzi wa hospitali na utoaji wa huduma za afya, badala ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi.
“Nionavyo, ufanisi mkubwa upo ZHC. Wizara mjikite kwenye hospitali, nyumba ziendelee kujengwa na shirika husika,” amesisitiza.
Akizungumzia maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Mwinyi amesema miradi mingi ya maendeleo inaendelea kufunguliwa, ikiwa ni ushahidi wa kazi kubwa inayofanyika katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, barabara, maji, viwanja vya ndege na bandari.
Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Hamida Mussa Khamis, amesema changamoto kubwa iliyokuwapo awali ilikuwa ni umbali kati ya hospitali na makazi ya wahudumu wa afya.
Amesema kukamilika kwa nyumba hizo ni hatua muhimu itakayohakikisha wananchi wanapata huduma za afya wakati wote.
“Madaktari walikuwa wanajitahidi, lakini umbali ulikuwa changamoto. Sasa hakuna sababu ya wananchi kukosa huduma wakati wowote,” amesema.