Msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric, amesema kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini New York, Marekani kwamba marekebisho hayo yanalenga kuzidisha kuzuia uwezo wa UNRWA kufanya kazi na kutekeleza majukumu yake yaliyoidhinishwa. 

“Sheria hiyo na marekebisho yake yamekuwa kinyume na hadhi ya UNRWA na mfumo wa kisheria wa kimataifa unaotumika kwa shirika hilo, na yanapaswa kufutwa mara moja,” amesema Katibu Mkuu kupitia taarifa hiyo.

Guterres amesema UNRWA ni sehemu muhimu ya Umoja wa Mataifa, na kwamba kwamba Mkataba wa Haki na Kinga za Umoja wa Mataifa unaendelea kutumika kwa UNRWA, mali zake, rasilimali zake, maafisa na wafanyakazi wake, na kwamba kutokukiukwa kwa mali yake hakupaswi kukiukwa.

Katibu Mkuu amerejelea wajibu wa Israel chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Haki na Kinga.

Taarifa hiyo kwa  vyombo vya habari imeongeza kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, katika maoni yake ya ushauri yaliyotolewa tarehe 22 mwezi Oktoba 2025, ilihitimisha kuwa Israel ina wajibu wa kuhakikisha heshima kamili ya haki na kinga zinazohakikishwa kwa Umoja wa Mataifa, ikiwemo UNRWA, na wafanyakazi wake ndani na kuhusiana na Eneo la Palestina Lililokaliwa.

Katibu Mkuu amesisitiza tena uungaji mkono wake mkubwa kwa UNRWA, ambayo ina jukumu lisiloweza kuepukika katika kuwahudumia watu wa Palestina huko Gaza na maeneo mengine ya kanda hiyo.

“Shughuli zinazoendelea za UNRWA huko Gaza zinachangia utekelezaji madhubuti wa Azimio la Baraza la Usalama namba 2803 na mpango mpana wa kumaliza mgogoro wa Gaza kwa vitendo, “ imetamatisha taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *