Katibu Mkuu wa Majlisi ya Uamsho ya Kiislamu Duniani amesema kuwa, maadui wa Iran walikosea sana katika mahesabu yao juu ya nguvu za kijeshi za Jamhuri ya Kiislamu, kwani makombora yenye usahihi mkubwa ya Iran yalipenya safu nyingi za mifumo ya ulinzi na kupiga kwa usahihi shabaha zilizokusudiwa, na kubadilisha kikamilifu mlingano wa nguvu katika eneo.

Katika ujumbe alioutoa kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa sita wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Velayati alisisitiza jana Jumanne kwamba, utawala wa Israel na washirika wake walikosea sana kwa kudunisha uwezo wa kijeshi wa Iran wakati wa vita vya siku 12 vya Juni mwaka huu 2025, vilivyoanzishwa na Wazayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

“Usahihi wa makombora ya Iran kupenya tabaka nyingi za mifumo ya hali ya juu ya ulinzi na kupiga shabaha nyeti katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kimsingi zilibadilisha mlingano wa nguvu, na kulazimisha adui kuomba kusitishwa kwa mapigano,” amesema Dakta Velayati.

Akiwahutubia wanazuoni, wasomi na shakhsia wa kisiasa, Velayati amesema vita hivyo havikuwa tu makabiliano kati ya Iran na utawala wa Kizayuni Israel, bali ni kampeni pana inayoungwa mkono na NATO na ushiriki wa moja kwa moja wa Marekani. “Mashambulizi hayo, yaliyolenga vituo vya nyuklia vya Iran, yaliunga mkono hatua za awali za Marekani katika Ghuba ya Uajemi wakati wa urais wa Ronald Reagan,” ameeleza Velayati.

Kadhalika Dakta Velayati ambaye pia ni Mshauri huyo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa  ameashiria ushawishi wa kimkakati wa Iran katika eneo la Asia Magharobo, akitaja kushindwa huko nyuma kwa Marekani na Israel katika nchi za Iraq, Lebanon, Palestina, Yemen na Syria, pamoja na tawala hizo za kishetani kutekeleza mauaji ya Jenerali Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Iraq Abu Mahdi al-Muhandis, na viongozi wengine muhimu wa mrengo wa Muqawama.

Aidha afisa huyo mwandamizi wa Iran ameusifu uongozi thabiti wa Jamhuri ya Kiislamu chini ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kwa kudumisha umoja wa kitaifa, kuimarisha uwezo wa kiulinzi, na kubatilisha majaribio ya kuunda ombwe la uongozi hapa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *