
Dar es Salaam. Ikiwa imesalia siku moja kabla ya kuanza mwaka mpya 2026, wataalamu wa siasa, uchumi na viongozi wa dini, wameutathmini mwaka 2025 kama mwaka ulioliacha taifa na doa la kisiasa.
Viongozi na wataaalamu sambamba na wachambuzi hao wanasema wanatamani kuona 2026 unakuwa na mwanzo mzuri wa kuzaliwa Tanzania mpya yenye kutoa haki, amani na mshikamano thabiti kwa watu wake.
Doa hilo, kwa mujibu wa wachambuzi hao, linatokana na maandamano yaliyozaa vurugu Oktoba 29, 2025 siku ya Uchaguzi Mkuu wa na kusababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali za umma na binafsi, hali iliyotikisa taswira ya nchi kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Kutokana na matukio hayo, mashirika mbalimbali ya kimataifa ndani na nje ya nchi, yametaka uwajibikaji kuhusu yaliyojiri siku hiyo.
Hata hivyo, tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshaunda Tume inayochunguza chanzo cha vurugu hizo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tume hiyo, Rais Samia alisisitiza kuwa jukumu kuu la Tume ni kuchunguza kwa kina chanzo cha matatizo yaliyojitokeza.
“Tume tunaitarajia itatuangalia sababu hasa iliyoleta kadhia ile; kiini cha tatizo ni nini?” aliagiza Rais Samia.
Akizungumza na Mwananchi juu ya kadhia hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Maimbo Mndolwa amesema sikukuu za Krismasi na mwaka mpya hubeba mafundisho mawili muhimu kwa taifa.
Amesema fundisho la kwanza ni uvumilivu katika nyakati ngumu, akitolea mfano wa Yusuph na Mariam kama inavyoelezwa katika maandiko ya matakatifu.
Askofu huyo wa Dayosisi ya Tanga amesema yaliyotokea mwaka 2025 tayari yamepita, lakini yanatoa ishara kuwa mbele kuna nuru. Amewashukuru wote waliovumilia changamoto na kuwapa pole walioumia, akisema huo ndio mwendo wa kuelekea mabadiliko chanya.
Fundisho la pili, amesema ni utayari wa kuhudumu na kushirikiana kwa pamoja licha ya misukosuko. Ametoa mfano wa Yusuph na Mariam ambao licha ya kusemwa vibaya, waliendelea kuwa pamoja hadi kuzaliwa kwa mtoto Yesu Kristo.
“Tunatamani kuzaliwa kwa taifa jipya baada ya tuliyopitia. Tangu tulipoanza kupigania uhuru hadi hapa tulipofika ni pakubwa. Magumu yaliyotokea yatuonyeshe kwamba taifa linaelekea kuzaliwa upya,” amesema askofu huyo.
Mtaalamu wa siasa, Dk Richard Mbunda kwa upande wake amesema mwaka 2025 umeandika historia hasi kutoka na namna uchaguzi ulivyoacha majeraha makubwa kwa wananchi na Serikali.
“Ni mwaka wa uchaguzi ulioliacha taifa na vidonda vikubwa. Tanzania ilikuwa mfano wa kuigwa katika demokrasia na uchaguzi wa amani, kiasi cha nchi nyingine kuja kujifunza kwetu,” amesema mchambuzi huyo.
Amesema machafuko ya uchaguzi yameitikisa taswira hiyo. “Tumetetereka sana kiasi kwamba yale majigambo ya watu kuja kujifunza kwetu sasa yana ukakasi,” amesema.
Dk Mbunda amesema siasa huathiri sekta karibu zote, akitaja utalii kuwa miongoni mwa zilizoyumba tangu kutokea kwa vurugu hizo.
Amesema hata maandamano yaliyotangazwa Desemba 9, 2025 ambayo hayakuwepo, pia yalisababisha watu kuahirisha safari na kusitisha shughuli mbamlimbali za kiuchumi na kusalia majumbani, hali iliyosababisha hasara.
“Siasa ni kama mboni ya jicho, ukichezea kidogo sekta zote zinatikisika,” amesema Mbunda.
Kwa upande wa wafanyabiashara, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT–Taifa), Khamisi Livembe amesema licha ya mwaka 2025 kushuhudia ukuaji wa biashara, athari kubwa zimekuja kujitokeza wakati ukielekea ukingoni.
“Shughuli nyingi zilifungwa, watu waliogopa kununua bidhaa, usafirishaji nao ulipata mtikisiko na wafanyabiashara wakapata hasara,” amesema.
Lakini Livembe amesema wanatarajia mwaka 2026 kuwa na ukuaji mkubwa wa biashara endapo hali ya kisiasa itaendelea kuwa shwari.
Naye Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Joseph Selasini amesema mwaka huu ulianza kwa matumaini baada ya kuundwa kwa kikosi kazi cha kisiasa.
“Tuliona dalili njema kwamba yaliyoahidiwa yangetekelezwa. Sheria zilipelekwa bungeni, lakini hazikukidhi matarajio ya wadau,” amesema.
Selasini amesema mvutano wa kisiasa uliendelea hadi uchaguzi ulipofanyika, huku matumaini ya marekebisho yakisalia hewani.
“Pamoja na kelele nyingi, hakuna kilichopatikana. Uchaguzi umeacha doa litakaloufanya mwaka 2025 kutosahaulika,” amesema Selasini.
Ameongeza kuwa matukio hayo yamefunika mafanikio mengine yaliyofanywa na Serikali na ya kitaifa, ikiwemo kukanilika kwa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere lililoongeza uzalishaji wa umeme nchini.
Kwa mtazamo wa kijamii na kielimu, mwandishi wa vitabu, Richard Mabala amesema mwaka huu unamalizika kwa majonzi, badala ya kuendelea kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa Watanzania, umezaa uhasama na vifo.
“Natamani mwaka ujao sababu zilizosababisha hali hii itokee zishughulikiwe kwa nguvu na turudi kwemye umoja wetu kama awali,” amesema Mabala.
Akizungumzia mtizmo wake katika elimu kwa 2025, Mabala amesema changamoto bado ni ile ile ya mfumo wa ufundishaji, hususan matumizi ya lugha na shinikizo la mitihani.
“Watoto wanatoka alfajiri kwenda shule na kurudi usiku, kiafya hili si sahihi.
Natamani mwaka 2026 uwe mwaka wa mageuzi ya elimu,” amesema.
Akizungumzia kwa ujumla wake, Mabala amesema mwaka 2025 umeacha funzo kubwa kwa taifa, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, mazungumzo ya dhati na mshikamano ili mwaka 2026 uwe mwanzo wa ukurasa mpya wa amani mshikamano na maendeleo.