Arusha. Zaidi ya wananchi 500 wa Mkoa wa Arusha wamenufaika na huduma ya uchunguzi na matibabu bure ya magonjwa ya moyo yanayotolewa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kupima afya zao mapema.
Akizungumza leo Jumatatu, Desemba 31, 2025, wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo, Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema mwitikio wa wananchi umeendelea kuwa mkubwa tangu kuanza kwa kambi hiyo Desemba 29, 2025, huku wananchi wakiendelea kupata matibabu kulingana na hali ya mgonjwa husika.
Amesema kambi hiyo inayotarajiwa kuhitimishwa Januari 5, 2026 imefanikisha uchunguzi kwa zaidi ya wananchi 500, ambapo wagonjwa 15 wamepata rufaa ya kufanyiwa matibabu ya kibingwa zaidi katika Hospitali ya JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam. Aidha, kati ya watoto 36 waliofanyiwa vipimo, watatu watapelekwa JKCI Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa kuzibwa matundu kwenye mioyo yao.
“Mwitikio wa wananchi kuja kufanyiwa uchunguzi umekuwa mkubwa, jambo linalotupa furaha kubwa kuona elimu tunayotoa kupitia vyombo vya habari imepokelewa kwa njia chanya. Wananchi wanaanza kuona umuhimu wa kufahamu hali zao za afya ili kuanza matibabu mapema,” amesema Dk Kisenge.
Ameeleza kuwa utoaji wa huduma hizo unafanywa kwa ushirikiano na Bohari ya Dawa (MSD) na kuwahakikishia wananchi wa Arusha na mikoa jirani kuwa, JKCI itaendelea kushirikiana na Hospitali ya ALMC, inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, katika kuimarisha huduma za afya ya moyo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk.Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 31, 2025 wakati wa kambi ya uchunguzi na matibabu ya bure katika hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) jijini Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu
Dk Kisenge ameongeza kuwa lengo la ushirikiano huo ni kuifanya hospitali hiyo kufikia malengo yaliyokusudiwa wakati inaanzishwa, ikiwemo kuwa kituo kikubwa cha huduma za afya za kibingwa kwa kuweka vifaa vya kisasa vya uchunguzi na tiba, kama ilivyo katika Hospitali ya JKCI jijini Dar es Salaam.
“JKCI imekuwa na ushirikiano mzuri na vyombo vya habari. Tunaamini mtaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kupunguza athari za magonjwa ya moyo kwa kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara na unene uliokithiri. Natoa wito kwa wananchi kutumia hospitali hii kupata huduma walizokuwa wakizifuata JKCI Dar es Salaam,” amesema.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya ALMC, Dk Goodwill Kivuyo, ameishukuru Serikali kwa kutekeleza sera ya kushirikiana na taasisi za kidini katika kuleta huduma za afya karibu zaidi na wananchi, hatua ambayo imechangia kuboresha utendaji wa hospitali hiyo kwa ujumla.
Amesema hospitali hiyo inakusudiwa kuwa kituo cha pamoja (One Stop Center) kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo pamoja na huduma nyingine, ikiwemo mifupa, upasuaji wa jumla, magonjwa ya ndani na huduma za watoto, huku maabara na huduma za mionzi zikiboreshwa kwa kuwekewa vifaa vya kisasa.
Naye mkazi wa Karatu, Paulina Awee, pamoja na Monica Chang’ah wa jijini Arusha, ambao walipata huduma za uchunguzi na matibabu bure, wameushukuru uongozi wa hospitali hiyo kwa huduma walizopata na kuomba kambi za uchunguzi wa magonjwa ya moyo ziendelee kufanyika mara kwa mara ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.