YANGA imepunguza mastaa wawili wa kigeni katika kikosi ilichonacho na kuingiza mashine mbili za kazi ikipiga hesabu za muda mfupi kuboresha kikosi hicho kwa ngwe ijayo ya michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Bara.

Iko hivi. Yanga itawasajili viungo wawili na wote watatokea Singida Black Stars wa kwanza ni Marouf Tchakei, raia ya Togo  ambaye anatua kwa mabingwa kama suluhisho la haraka kama kiungo mshambuliaji namba 10.

Awali Yanga ilikuwa inamtaka Allan Okello wa Uganda, lakini bosi wa klabu ya Vipers kama ambavyo Mwanaspoti lilikujulisha kwamba jamaa amegoma kupokea Dola 120,000 kumuachia.

Okello alishakubali kutua Yanga na kila kitu kilikuwa kimekamilika kwa upande wa mchezaji, lakini bosi wa juu kabisa wa klabu yake akaweka ngumu na kuifanya wababe hao wa Tanzania kusaka mbadala wa haraka ili mambo yasiwaharibikie wakati dirisha dogo likifungiliwa rasmi leo na kutarajiwa kufungwa Januari 31.

Hata hivyo, Yanga na Okello wamekubaliana kwamba wataurudisha usajili huo mara baada ya msimu kumalizika ambapo atakuwa ameshamaliza mkataba wa miezi sita na Vipers.

Tchakei ni kiungo mzoefu ambaye anajua kutekeleza majukumu yake ipasavyo huku pia akiwa na ufundi wa kujua kupiga mipira iliyokufa. Ujio wa Tchakei raia wa Tigo, unamuondoa Mamadou Doumbia anayekwenda Singida na kiungo huyo hana shida amekubali maamuzi hayo yaliyomhakikishia malipo yake ya kimkataba kuendelea.

Mbali na Tchakei rasmi Yanga itamchukua Damaro Camara kiungo mkabaji wa chini akitokea palepale Singida.

Damaro alikubali haraka kuja Yanga, lakini Singida ikawa inasita kumuachia kutokana na hali ya Khalid Aucho ambaye amekuwa na nyakati za kuwa majeruhi.

Yanga ilikuwa inampigia hesabu Damaro kwa muda mrefu, lakini haikufanikiwa na sasa dili hilo limetimia na anajiunga na mabingwa hao haraka kupitia dirisha dogo la usajili na dili lake limekuja kutokana na klabu hiyo kukutana na ugumu wa kumpata kiungo wa kazi raia wa Madagascar Nicolas Rijaniaina.

Kama ilivyokuwa kwa Okello, ndivyo ambavyo Rijiniaina alivyowekewa kauzibe na klabu yake ya Al Merreikh ikisema ni vigumu kumuachia kwa sasa labda mwisho wa msimu. Ujio wa Damaro unamng’oa Moussa Balla Conte ambaye alishindwa kuonyesha makali na Sasa atakwenda kujiuliza akiwa pale Singida Black Stars.

Awali Yanga ilikutana na presha wakati wa kumuondoa Conte, Mwanaspoti linafahamu kwamba kiungo huyo aligoma kutoka kwa mkopo kabla ya mabosi wa juu kumaliza kitu kwenye dili hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *