
Chapisho la makadirio ya mwelekeo wa upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2026 lililotolewa leo na WFP linaonya kuwa, mbali na njaa inayoshuhudiwa katika kipindi hiki, dunia pia inakabiliwa na hali ya ukosefu wa virutubisho muhimu— inayowaathiri vibaya mabilioni ya watu, kudhoofisha mifumo ya afya, kudumaza ukuaji wa uchumi na kuendeleza mizunguko ya umaskini na kuyumba kwa utulivu wa kijamii.
Kwa mujibu wa chapisho hilo, takribani watu milioni 318 wanakabiliwa na njaa kali, idadi iliyo mara mbili ya ilivyokuwa kabla ya janga la coronavirus“>COVID-19. Kati yao, watu milioni 41 wapo katika kiwango cha 4 cha dharura cha ukosefu wa chakula.
Halikadhalika njaa kali imethibitishwa katika maeneo ya Ukanda wa Gaza huko Mashariki ya Kati, na sehemu za Sudan, ikiwa ni mara ya kwanza katika karne hii kwa njaa kutokea katika maeneo mawili kwa wakati mmoja.
Ripoti imebainisha maeneo 16 yaliyo hatarini kukumbwa na njaa kali ikiwemo Haiti, Mali, Afghanistan na Yemen. Mizozo vya kivita inachangia asilimia 69 ya njaa duniani, huku athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi — ikiwemo ukame, mafuriko na dhoruba — zikiongeza makali ya mgogoro wa chakula.
Nchini Syria, uzalishaji wa mazao umepungua kwa asilimia 60, huku Kimbunga Melissa kikisababisha uharibifu mkubwa katika Jamaica, Haiti na Cuba.
Kuna matumaini katika changamoto
Hata hivyo, ripoti hiyo imeonesha pia dalili za matumaini. WFP inalenga kufikia idadi ya watu milioni 110 mwaka 2026, kwa mahitaji ya kiutendaji ya takribani kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 13. Ubunifu na ushirikiano ni nguzo muhimu za juhudi hizo, ambapo zana za Akili Mnemba kama SCOUT zinaboresha minyororo ya usambazaji na kuokoa mamilioni ya dola.
Aidha, uhawilishaji wa fedha kwa njia ya kidijitali na utekelezaji wa hatua za mapema husaidia kulinda maisha kabla ya majanga kutokea — ambapo kila kiasi cha dola inayowekezwa huokoa hadi dola saba za hasara.
WFP imesisitiza kuwa ina rasilimali watu wenye utaalamu na uzoefu wa kina katika utekelezaji wa miradi katika maeneo husika, jambo linalohakikisha kila kiasi cha dola kinachochangwa kinaleta matokeo chanya yenye tija.
Shirika hilo limetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwekeza katika suluhu zilizothibitishwa ili kudhibiti kuenea kwa njaa na kurejesha dunia katika mwelekeo wa kufikia lengo la kutokomeza njaa ifikapo mwaka 2026.