BUKOBA: Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhandisi Johnston Mtasingwa, amekabidhi jumla ya magodoro 20 kwa Kituo cha Vipaji cha Tyaido Academy kilichopo Kata ya Buhembe, Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera.

Msaada huo umetolewa kufuatia ombi maalumu lililowasilishwa kwa mbunge kwa lengo la kusaidia maendeleo ya vipaji vya vijana wanaolelewa katika kituo hicho.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo kwa niaba ya Mbunge, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Hamad Simba, amesema kuwa dhamira ya Mbunge ni kukisaidia kituo hicho kiendelee kutimiza malengo yake ya kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana.

Aidha, ameahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu kati ya ofisi ya mbunge na uongozi wa Tyaido Academy.

Uongozi wa kituo hicho umeushukuru msaada huo na kueleza kuwa utasaidia kuboresha mazingira ya malezi na maendeleo ya vijana waliopo kituoni hapo.
