Baraza la Makanisa Duniani (WCC) limeutaka Umoja wa Ulaya (EU) kuiwekea Israel vikwazo na vikiwemo vya silaha kutokana na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza, na ukiukaji wa haki dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu.

Iskandar Majlton, Mratibu wa Mipango wa baraza hilo huko Palestina na maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel amesema msimamo wa WCC umejikita katika sheria za kimataifa na haki za binadamu.

“Baraza hili lilishtushwa sana na wimbi la ghasia na mateso makubwa katika eneo hilo,” ameeleza Majlton na kuongeza kuwa, Gaza inakabiliwa na “janga la kibinadamu ambalo halijawahi kutokea.

“Msururu wa kutisha wa vurugu” haukuanza Oktoba 2023, lakini ni matokeo ya miongo kadhaa ya uvamizi, vikwazo vilivyowekewa Gaza, na ukosefu wa usawa wa kimfumo, amesema afisa huyo wa Baraza la Makanisa Duniani.

Onyo hilo limekuja huku afisa mkuu wa Umoja wa Ulaya katika masuala ya kibinadamu, Hadja Lahbib akionya kwamba, tishio la Israel la kusimamisha makundi kadhaa ya misaada huko Gaza kuanzia Januari linaweza kuzuia misaada ya “kuokoa maisha” kuwafikia wakazi. 

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Stephane Dujarric,amelaani marekebisho ya sheria yaliyopitishwa na Bunge la utawala wa kizayuni wa Israel, Knesset Desemba 29, yanayohusu kusitishwa shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA). akieleza kuwa, marekebisho hayo yanalenga kuzuia UNRWA kufanya kazi na kutekeleza majukumu yake yaliyoidhinishwa. 

Nayo Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina imeripoti kuwa, mwaka 2025 ulikuwa mwaka mbaya zaidi katika uga wa kibinadamu na idadi ya jamii ya watu huko Palstina kutokana na vita vya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kuongezeka kwa ukiukaji wa haki katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na Quds Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *