#HABARI: Mkuu wa Wilaya ya Kahama Bw. Frank Nkinda amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanaweka mkazo watoto wao kwenda shule, akidai kuwa Kahama imekuwa na changamoto kubwa ya Mdondoko wa wanafunzi katika Shule za Msingi na Sekondari hali ambayo inasababishwa na malezi ya baadhi ya wazazi kutokidhi vigezo vya maadili kwa watoto wao.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Frank Nkinda, ameyasema hayo katika ibada maalum ya kuliombea Taifa la Tanzania Amani na Utulivu, iliyoandaliwa na Askofu wa Kanisa la Ufunuo Mkoa wa Shinyanga Askofu Samawi Alex Bendela Nyasubi Wilayani Kahama.
Aidha, Askofu Samawi Alex Samawi amesema malengo ni kuombea nchi iwe na utulivu huku akikemea wazazi kuwaruhusu watoto wadogo kutumia simu janja kwakuwa inaweza kuwa kichocheo cha kuporomoka kwa maadili.
Nao baadhi ya wazazi walioshiriki ibada hiyo wamesema wameupokea mwaka mpya 2026 kwa Moyo Mmoja na matarajio yao ni kuwa na mwaka wenye mafanikio makubwa kiuchumi ambapo wameiomba Serikali kuhakikisha changamoto zinaikabili jamii zinatatuliwa.