Katika kuadhimisha sherehe za kufunga mwaka 2025 na kufungua mwaka mpya wa 2026, Hifadhi ya Taifa Mikumi imeendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii wa ndani baada ya kutembelewa na Godfrey Rugalabamu, maarufu kama Mc Gara B, mdau wa utalii na mwanamitandao mwenye ushawishi mkubwa nchini Tanzania, aliyeambatana na familia yake kushiriki shughuli mbalimbali za kiutalii. Uwepo wake Mikumi umebeba ujumbe mpana wa kuhamasisha Watanzania kuthamini na kuchagua vivutio vya ndani kama sehemu ya maisha na utamaduni wa Taifa.
Hatua hiyo inaenda sambamba na juhudi za Ofisi Kiunganishi ya TANAPA Dar es Salaam, iliyopo katika jengo la Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) mkabala na Ubalozi wa Ufaransa, ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kuratibu, kutoa taarifa na kusimamia huduma kwa wageni, wadau wa utalii na Watanzania kwa ujumla. Ofisi hiyo hutoa elimu kuhusu Hifadhi za Taifa, husaidia maandalizi ya safari, uratibu wa makundi ya watalii, mawasiliano ya kitaalamu pamoja na kampeni mbalimbali za kuhamasisha utalii wa ndani na nje, ikiwa ni kiungo muhimu kati ya TANAPA, sekta binafsi na jamii.
Kwa ujumla, uwepo wa watu wenye ushawishi kama Mc Gara B katika Hifadhi za Taifa ni ushahidi wa nguvu ya majukwaa ya kidijitali katika kukuza taswira chanya ya utalii wa Tanzania. Ushirikiano huu kati ya wadau, TANAPA na jamii unaendelea kuimarisha ulinzi wa rasilimali za asili, kuongeza idadi ya watalii wa ndani na kuchochea ukuaji wa utalii endelevu unaochangia moja kwa moja katika uchumi wa nchi.
#kilichoborakabisa