London, England. Safari kutoka Hull City hadi Chelsea kupitia Strasbourg huenda isimfanye Liam Rosenior kuingia kwenye orodha ya makocha wenye majina makubwa ambao walikuwa wakitajwa kujiunga na miamba hiyo ya soka England baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Enzo Maresca kuachishwa kazi.

Hata hivyo, hadi sasa kwenye makaratasi kocha huyo ndiye mgombea anayeongoza kumrithi Maresca katika benchi la ufundi la Chelsea jambo linalowashangaza wengi.

Huyu ni kocha mwenye umri wa miaka 41 tu, aliyefukuzwa na Hull City miezi 19 iliyopita licha ya kuteuliwa kuwania tuzo ya Kocha Bora wa Championship. Kocha aliyepitia vurugu, presha na kutotabirika kwa soka la kisasa. Inaonekana kama sifa kamili kwa kazi yenye presha kubwa Stamford Bridge.

Kutakuwa na wale watakaobeza hata wazo la Rosenior kutajwa kama kocha wa Chelsea, wakisisitiza kuwa hajawahi kuinoa timu ya Ligi Kuu England. Lakini pia wapo wanaomuona kama kocha mwenye kipaji cha kipekee.

Huenda dalili hizo zilianza kuonekana alipokamilisha leseni yake ya UEFA A akiwa na umri wa miaka 32 wakati akiwa bado mchezaji. Au wakati alipomsaidia Wayne Rooney kukabiliana na machafuko ya klabu ya Derby County iliyokuwa kwenye mgogoro mkubwa wa kifedha.

Hata hivyo, ni Hull City ndiko Rosenior alipopata nafasi ya kuweka jina lake mlangoni na kuwafanya wengi waanze kumzungumzia. Ndani ya miezi 18 tu, aliibadilisha Hull City kutoka timu ya kupambana kuepuka kushuka daraja hadi kuwa wapinzani wa kupanda Ligi Kuu.

Alifanya hivyo kwa mtindo wa kuvutia. Wakati Hull City walipokuwa katika ubora wao, walicheza soka la kasi, pasi za uhakika na mpangilio wa timu uliovutia macho ya mashabiki wengi. Walikuwa jasiri katika kushambulia na vivyo hivyo katika kujilinda, mara nyingi walicheza ili kuwanyima wapinzani nafasi.

Rosenior, ambaye ni shabiki wa Manchester United tangu utotoni, anamuenzi Sir Alex Ferguson kama shujaa wake. Hata hivyo, ni Pep Guardiola anayemtaja kama aliyemshawishi zaidi kiufundi, na hilo linaonekana wazi katika timu zake.

Akiwa Hull City na baadaye Strasbourg, Rosenior amejijengea sifa kubwa kama kocha mahiri wa kukuza vipaji vya vijana. Tyler Morton, Jaden Philogene na Liam Delap wote walionyesha makali yao kwa mara ya kwanza katika soka la wakubwa chini yake. Aidha, alimrudisha Fabio Carvalho kwenye ubora wake baada ya kupotea benchi Liverpool.

Sio vijana pekee waliofaidika. Wachezaji wenye uzoefu wa Ligi za chini England pia waliinuliwa kiwango chao. Hili linahusishwa zaidi na uwezo mkubwa wa Rosenior katika akili ya kihisia. Wachezaji wake walipenda kufanya kazi naye. Alijua lini amtulize mchezaji na lini amwambie ukweli mchungu. Chelsea wamewahi kudai Maresca alikosa ukomavu wa kihisia shutuma ambayo haziwezi kabisa kuelekezwa kwa Rosenior.

Hata hivyo, mwisho wa msimu, Hull City ya Rosenior ilishindwa kudumisha kasi katika mbio za kupanda daraja. Waliporomoka mwishoni mwa msimu na kukosa nafasi ya kucheza mechi za mtoano.

Mmiliki wa Hull City, Acun Ilicali, alitaja soka la kuchosha kama sababu ya kumfuta kazi Rosenior, badala ya kukosa kupanda daraja. Kwa nyakati fulani, mfumo wake wa umakini na nidhamu ulionekana mzito na wa polepole. Siku ambayo haukufanya kazi, alilaumiwa kwa kukosa kubadilika kiufundi. Lakini Rosenior angeona hilo kama uaminifu kwa falsafa yake, si ukaidi.

Kuhamia Strasbourg kuliwashangaza wengi, lakini ilikuwa hatua ya busara kwake kujiingiza ndani ya mtandao wa BlueCo wanaomiliki Strasbourg na Chelsea. Lengo lake ilikuwa kwamba siku moja angeinoa timu ya Ligi Kuu England jambo ambalo linaweza kutokea muda wowote kwanzia sasa.

Kufuzu kucheza soka la Ulaya akiwa kocha kwa mara ya kwanza nje ya England, huku kukiwa na hali ya sintofahamu kwa mashabiki, lilikuwa jambo kubwa. Alifanikiwa kwa kushikilia misingi yake: kuwaamini vijana na kucheza soka la kushambulia kwa ujasiri jambo linalolingana na wasifu wa kikosi cha Chelsea.

Hata hivyo, kazi ya kuinoa Chelsea italeta changamoto ambazo hajawahi kukutana nazo: mastaa wenye majina makubwa na matarajio makubwa zaidi. Safari ya Graham Potter, kocha wa mwisho Mwingereza kuinoa Chelsea, ni onyo tosha la namna mambo yanavyoweza kuharibika.

Lakini Rosenior si mtu wa kukosa msimamo. Inatosha kusikiliza hotuba zake za chumba cha kubadilishia nguo zilizosambaa mitandaoni kutambua hilo.

Mwisho wa siku, mafanikio yake Stamford Bridge yatapimwa kwa mataji. Hajawahi kupambana na presha ya kushinda vikombe wala changamoto zinazokuja pamoja na hilo.

Iwapo atapewa kazi hiyo, itakuwa mtihani mkubwa wa uwezo na uthubutu wake. Lakini ni mtihani ambao Rosenior haonekani kuogopa kuikabili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *