
London, England. Enzo Maresca ameondoka Chelsea baada ya matukio matano muhimu kusababisha kuvunjika kwa uhusiano wake na klabu hiyo.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 alifukuzwa kazi Siku ya Mwaka Mpya baada ya wiki kadhaa za sintofahamu, msongo wa mawazo na kuchanganyikiwa ndani ya klabu, licha ya kushinda mataji mawili msimu uliopita. Kinachoelezwa kuna mambo matano yamechangia hilo.
1. Mazungumzo na Man City; Vyanzo vya Chelsea vimemtuhumu Maresca kwa kufanya mazungumzo ya siri na Manchester City kuhusu uwezekano wa kuchukua nafasi ya Pep Guardiola huko Etihad. Hilo limemfanya afunguliwe mlango wa kutokea Stamford Bridge.
2. Mgogoro na timu ya madaktari; Maresca hakutoa maelezo kwa wafanyakazi wa klabu waliokuwa wamechanganyikiwa, wala hakufanya hivyo hadharani. Hata hivyo, vyanzo vinaamini mgogoro huo ulihusu ushauri wa kitabibu kuhusu muda salama wa kuwachezesha wachezaji. Inaelezwa Maresca alipuuza ushauri wa madaktari kuhusu muda salama wa wachezaji kukaa uwanjani, na aliwaacha kucheza kwa muda mrefu zaidi akilenga kupata matokeo. Moises Caicedo na Enzo Fernández wamecheza sehemu kubwa ya msimu huu huku wakisumbuliwa na majeraha madogo madogo.
3. Kauli za hadharani; Kauli ya Maresca kuhusu “saa 48 mbaya zaidi” haikuwa shambulizi pekee la kificho dhidi ya klabu katika wiki za hivi karibuni. Baada ya mkutano na waandishi wa habari kufuatia mechi dhidi ya Bournemouth, vyanzo vya klabu vilisema kauli zake zilikuwa “mwitikio wa kihisia baada ya ushindi wa kihisia”. Hata hivyo, katika mkutano uliofuata, Maresca alisisitiza wazi kuwa kauli yake haikuwa ya kihisia bali ilikuwa imepangwa mapema kwamba kuna mambo yanaendi vizuri chini ya mabosi wa Chelsea.
4. Matokeo mabaya; Hili ndilo jambo ambalo hatimaye humgharimu kocha yeyote kazi. Kama Maresca angekuwa anakosoa sera za klabu hadharani huku akipata ushindi wa mfululizo, huenda viongozi wasingeweza kuchukua hatua ya kumfuta kazi. Lakini, mechi kadhaa bila ya ushindi uliwafanya mambo kuchoka na kumfungulia mlango wa kutokea.
5. Kukwepa mkutano wa waandishi wa habari; Hili ndilo tukio lililoonekana kuwa baya zaidi, ambapo watu wa ndani ya Chelsea waliliona kama kukosa heshima kwa klabu na wafanyakazi.
Baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Bournemouth, Jumanne, msaidizi wake Willy Caballero alitumwa kukutana na waandishi wa habari badala ya Maresca, ambaye alidai hajisikii vizuri.