
Wakati mwaka 2026 ndio umeanza bara la Afrika na hasa eneo la Afrika Mashariki linatarajiwa kuendelea kushuhudia vurugu kama za mwaka uliopita, ambapo maelfu ya raia walipoteza maisha na wengine maelfu kuwa wakimbizi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mwaka uliopita mzozo wa Sudan, unatajwa kuwa moja ya migogoro mibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa kidunia, ambapo tangu kuanza kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe mwezi April mwaka 2023, maelfu ya raia wameuawa na mamilioni wamekuwa wakimbizi.
Mzozo wa taifa hili ukiorodheshwa sambamba na ule wa Ukraine, Syria na Gaza, kuwa moja ya migogoro mibaya zaidi duniani iliyosababisha janga la kibinadamu.
Kwa mujibu wa takwilu za umoja wa Mataifa, migogoro kwenye nchi za Afrika mashariki, ilizalisha wakimbizi zaidi ya milioni 7 na milioni 18 walikuwa wakimbizi wa ndani, wengi wakitokea Sudan.
Mzozo wa Sudan, umeiathiri pia Jirani yake Sudan Kusini ambayo tayari imepokea maelfu ya raia wa Sudan, wakati huu Juba yenyewe ikiwa na changamoto za kiusalama zinazotokana na kutotekelezwa kikamilifu kwa mkataba wa amani wa mwaka 2018.
Mzozo mwingine unaotajwa utagubika shughuli za mwaka huu ni ule wa mashariki mwa DRC, ambapo pamoja na utiwaji Saini wa mikataba kadhaa ya amani kati ya Serikali ya Kinshasa na waasi wa M23 na ule wa Kinshasa na Rwanda, bado raia wanaendelea kupoteza maisha na maelfu kukimbia makazi yao.
Kwa mujibu wa mashirika yanayofuatilia migogoro duniani, mizozo kwenye nchi ya Sudan, Ethiopia, Somalia, DRC, Nigeria na Burkina Faso, huenda ikasalia kuwa mibaya zaidi ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa kukomesha machafuko yanayoendelea.