Arsenal na Manchester City zinaendelea kuonekana kuwa timu mbili zenye nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2025/26, huku mwezi Januari ukitarajiwa kuwa kipimo muhimu cha ubora na uthabiti wao katika mbio hizo.
Mwaka mpya umeanza na kwa kawaida hilo humaanisha muda umeanza kuhesabiwa kuelekea siku ambayo kombe la Premier League litanyanyuliwa. Swali kubwa linalobaki ni timu gani itafanya hivyo.
Kwa sasa, Arsenal wanaonekana kuwa na nafasi nzuri zaidi. Kikosi cha kocha Mikel Arteta kimeanza msimu kwa kasi na ubora mkubwa, hali iliyodhihirika kupitia ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Aston Villa. Ushindi huo umewaacha The Gunners wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi nne mbele ya wapinzani wao wa karibu.
Iwapo wataendelea kushikilia nafasi hiyo hadi mwisho wa msimu, Arsenal watahitimisha zaidi ya miaka 20 ya kusubiri taji la ligi. Hata hivyo, changamoto kubwa bado ipo kwa Man City ambao wanaonekana kuwa wapinzani wao wa karibu.
Timu ya Pep Guardiola imezoea kutwaa ubingwa wa Premier, lakini jana imeanza mwaka 2026 vibaya baada ya kutoka suruhu dhidi ya Sunderland katika Uwanja wa Mwangaza.
Kadri kila raundi ya ligi inavyosogea, ndivyo mbio za ubingwa zinavyozidi kuchangamka. Hii hapa ratiba ya mechi tano zijazo za mwezi Januari kwa timu hizo mbili:
Licha ya majukumu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Carabao na FA, Arsenal inatarajiwa kuweka mkazo mkubwa kwenye mbio za ubingwa wa ligi.
Mechi yao ya kwanza ya mwaka 2026 itakuwa ugenini dhidi ya Bournemouth. Baada ya hapo, watakuwa na kibarua kigumu zaidi nyumbani dhidi ya mabingwa watetezi Liverpool. Ingawa kikosi cha kocha Arne Slot hakijawa katika ubora wake msimu huu, bado ni wapinzani hatari.
Baada ya mchezo huo, Arsenal wataifuata Nottingham Forest, kabla ya kuikaribisha Manchester United katika pambano la mwishoni mwa mwezi. Ratiba yao ya Januari itahitimishwa kwa mchezo wa ugenini dhidi ya Leeds United wanaoonesha dalili za kurejea katika makali yao ya zamani.
Manchester City
Kwa upande wa Manchester City, watakuwa na safari ya kwenda Stamford Bridge ambayo mara zote imekuwa ngumu, na hali hiyo inatarajiwa kuendelea. Hata hivyo, Chelsea wako bila kocha baada ya kuondoka kwa Enzo Maresca, jambo linaloweza kuifanya mechi hiyo iwe na sura tofauti.
Ratiba ngumu inaendelea ambapo City itawakaribisha Brighton katikati ya wiki, kabla ya kuelekea Old Trafford katika mchezo wa dabi ya Manchester dhidi ya United. Kisha watakuwa na nafasi nzuri ya kuvuna pointi tatu watakapowakaribisha Wolves walioko mkiani mwa msimamo wa ligi.
Mchezo wa mwisho katika ratiba hii ni safari ya kwenda Tottenham. Ingawa Spurs wamekuwa wakisumbua mara kwa mara kikosi cha Guardiola katika misimu ya nyuma, wengi wanaamini City bado wana nafasi ya kupata matokeo chanya.
Ratiba ya Manchester City:
Chelsea (Ugenini) – Jumapili, Januari 4
Brighton & Hove Albion (Nyumbani) – Jumatano, Januari 7
Manchester United (Ugenini) – Jumamosi, Januari 17
Wolverhampton Wanderers (Nyumbani) – Jumamosi, Januari 24
Tottenham Hotspur (Ugenini) – Jumapili, Februari 1
Ratiba ya Arsenal:
Bournemouth (Ugenini) – Jumamosi, Januari 3
Liverpool (Nyumbani) – Alhamisi, Januari 8
Nottingham Forest (Ugenini) – Jumamosi, Januari 17
Manchester United (Nyumbani) – Jumapili, Januari 25
Leeds United (Ugenini) – Jumamosi, Januari 31