“Jina langu ni Rafa Ahmed. Nina miaka 19 na ninatoka  Nubi, kaunti ya Kisii.”

Rafa Ahmed kutoka nchini Kenya anatuelezea kilichomkuta akiwa darasa la sita. 

“Mama yangu hakuweza kunilipia ada yangu ya shule, hivyo nililazimika kuacha masomo. Hali hii ilinifanya nitafute mvulana ambaye angeweza kunisaidia mimi na mama yangu, ili angalau tusibebe mzigo wa maisha. Baada ya kujifungua, nilitaka kutumia upangaji uzazi, lakini kwa wakati huo tulilazimika kulipa pesa, na mama hakuwa na fedha za kulipia ili nipate huduma ya upangaji uzazi.”

Ili kukabiliana na tatizo la mimba za utotoni, Mpango wa afya ya uzazi kwa barubaru au Adolescent Sexual and Reproductive Health Development Impact Bond unatumia jukwaa la Tiko kutoa bure elimu na huduma bora za afya ya uzazi na kijinsia, kuhakikisha wasichana wanapata huduma salama na kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya na maisha yao ya baadaye.

Hii ni kwa sababu mimba za utotoni husababisha wasichana kuacha shule, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi au HIV, na mzunguko wa umasikini unaozidi kushikilia kila kizazi.

Kwa wasichana wanaoishi katika umasikini, kupata huduma za afya si changamoto tu, bali ni kitu kisichowezekana. Anders Thomsen, Mwakilishi wa UNFPA Kenya, anasema

 “Katika mpango huu, wasichana 300,000 wamepangwa kupatiwa huduma kupitia vituo vya afya vya umma na binafsi katika kaunti kumi. Kaunti hizo zimetajwa kwa kuzingatia viwango vya juu vya mimba za utotoni na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.”

Mpango huo umeleta matokeo chanya kama anavyosimulia Rafa

“Huduma hizi zimesaidia wasichana wengi katika jamii yangu kuhitimu shule na kupunguza visa vya mimba za utotoni katika jamii.”

UNFPA inasema kuwa pindi wasichana wanapoungwa mkono, hawabaki tu kuishi katika umasikini, wanaupita na kuushinda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *