Nabii maarufu kutoka Ghana, Nigel Gaisie ametabiri kuwa timu ya taifa ya nchi hiyo, Black Stars, itafika fainali ya Kombe la Dunia la mwaka 2026.

Ghana, Mabingwa wa Afrika mara nne, itashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya tano katika historia yake. Mashindano ya mwaka 2026 yatafanyika kwa pamoja nchini Marekani, Canada na Mexico, ikiwa ni mara ya kwanza kushirikisha timu 48.

Black Stars imepangwa katika Kundi L pamoja na Panama, England na Croatia, kundi linaloonekana kuwa na ushindani mkubwa.

Akizungumza wakati wa Ibada ya 31 katika Kanisa lake la Prophetic Hill Church, Nabii Gaisie alionyesha imani kubwa juu ya safari ya Ghana katika mashindano hayo.

“Black Stars watafika fainali ya Kombe la Dunia 2026,” amesema kwa kujiamini, kauli ambayo tayari imezua mjadala mpana miongoni mwa mashabiki wa soka barani Afrika na duniani.

Ghana itaanza kampeni yake ya hatua ya makundi kwa kucheza dhidi ya Panama Juni 17 jijini Toronto, kabla ya kuvaana na England Juni 23 mjini Boston. Mechi yao ya mwisho ya kundi itakuwa dhidi ya Croatia Juni 27 huko Philadelphia.

Baada ya kuaga mashindano mapema katika Kombe la Dunia la Brazil mwaka 2014 na Qatar 2022, Black Stars wanaingia katika michuano hii wakiwa na hamasa kubwa ya kufuta kumbukumbu hizo na kuacha alama mpya, hasa katika mfumo mpya wa mashindano uliopanuliwa.

Katika maandalizi ya Kombe la Dunia, Ghana imepanga kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Ujerumani Machi 30 jijini Stuttgart, mchezo unaotarajiwa kuwa kipimo muhimu cha ubora wa kikosi hicho kabla ya kuingia rasmi katika mashindano.

Iwapo utabiri wa Nabii Gaisie utatimia, Ghana itakuwa imeandika historia mpya katika soka ikiwa ni timu ya kwanza ya Afrika kufikia hatua hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *