GEITA: SERIKALI imekamilisha kufunga mifumo ya kunasa radi katika shule 12 zilizopo wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya kuwalinda wananchi pamoja na wanafunzi dhidi ya ajali za radi.

Hatua hiyo inakuja kufuatia mfululizo wa matukio ya radi wilayani humo ikiwemo tukio la Januari 27, 2025 lililopelekea vifo vya wanafunzi saba na kujeruhi 82 katika shule ya sekondari Businda.

Mkuu wa wilaya ya Bukombe, Pasikasi Muragili ametoa taarifa hiyo katika mahojiano na waandishi wa habari na kueleza kuwa maboresho yanaendelea kabla ya shule kufunguliwa Januari 13, 2026.

Muragili amesema ili kufanikisha mpango huo serikali kupitia halmashauri hiyo imeweka mkakati wa kutenga fedha kidogo kidogo kila mwezi kwa ajili ya uwekaji wa mifumo ya kunasa radi.

Amesema mbali na maeneo ya shule serikali pia imeshatoa maelekezo kwa taasisi za umma na kijamii ikiwemo taasisi za kidini kuchukua hatua ya kuweka mifumo hiyo kwenye maeneo yao.

Amesema ili kufikia malengo serikali wilayani Bukombe inataraji kuanza ukaguzi katika taasisi zote ili kujionea utekelezaji wa suala hilo baada ya muda waliopewa ili kuepuka matukio ya ajali za radi.

“Taasisi zote za umma na kijamii zenye kuwa na watu wengi, tulifanya nao vikao na tulikubaliana na tuliwasisitiza wafanye hivyo,tulipeana muda na kwasasa tunakwenda kuanza ukaguzi”, amesema.

Ifahamike kuwa mkoa wa Geita ni miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa wahanga wa matukio ya ajali za radi ambazo zimetokea kwa miaka ya hivi karibuni hasa maeneo ya shule.

Ikumbukwe, mbali na tukio la shule ya sekondari Businda wilayani Bukombe, pia Oktoba 17,2018 wanafunzi sita wa shule ya msingi EMMACO Vision wilayani Geita walifariki dunia na wengine 23 kujeruhiwa.

Aidha tukio jingine la kusikitisha lilitokea Oktoba 18, 2019 wanafunzi 39 wa Shule ya msingi Ihumilo wilayani Geita walijeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa darasani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *