
Taarifa iliyotolewa jioni ya Ijumaa Januari 2 mwaka 2026 na msemaji wa Guterres inamnukuu akitoa wito wa hatua hiyo kubatilishwa, akisisitiza kuwa, “kazi za mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali kwenye eneo hilo ni muhimu katika kuokoa maisha ya binadamu.”
Amesema “kusitishwa kwa operesheni zao kunahatarisha maendeleo yaliyopatikana katika kipindi hiki cha sitisho la mapigano.”
Guterres ametanabaisha kwamba tangazo la Israeli la sitisho la shughuli za mashirika hayo linakuja wakati tayari kukiwa kuna vizuizi vya awali ambavyo vimeshasababisha “kucheleweshwa kuingizwa kwa vyakula muhimu, dawa, huduma za usafi na malazi huko Gaza, eneo linalokaliwa na Israeli.”
“Hatua hii ya hivi karibuni itaongeza zaidi janga la kibinadamu ambalo tayari linakabili wapalestina,” amesema Katibu Mkuu.
Amesisitiza kwamba kwa kuzingatia wajibu chini ya sheria ya kimataifa ya kiutu, “Israeli lazima iruhusu na ifanikishe uingizaji haraka na bila vikwazo vyovyote wa misaada ya kibinadamu inayohitajiwa na wapalestina wote.”
“Wadau wote wa kiutu ni lazima waweze kuendesha operesheni zao kwa usalama na kwa mujibu wa kanuni za kibinadamu,” amesema Guterres.