Askari wa gadi ya baharini ya Gambia wameopoa majini miili saba ya wahamiaji wasio na vibali, huku wengine 96 wakiokolewa kufuatia ajali ya boti pwani ya nchi hiyo.

Miili saba ilipatikana huku watu 96 waliokolewa baada ya boti iliyokuwa imebeba wahamiaji zaidi ya 200 kuzama usiku wa kuamkia jana huko kaskazini magharibi mwa Gambia.

Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ilisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, shughuli za utafutaji na uokoaji zingali zinaendelea. Ajali hiyo ilitokea karibu na kijiji cha Jinack, eneo la pwani la North Bank (Ukingo wa Kaskazini).

Hili lilikuwa tukio la hivi karibuni la mauti katika mojawapo ya njia hatari zaidi za wahamiaji duniani zinazotembelewa zaidi na Waafrika Magharibi wakijaribu kufika Uhispania kupitia Visiwa vya Canary.

Gambia ni moja ya njia zinazotumiwa na wahajiri haramu kutoka nchi mbalimbali hususan za Afrika kwa tamaa ya kufika Ulaya ambako wanadangaywa kuwa kuna maisha mazuri. 

Baadhi ya vijana wa Gambia wanaolazimika kuacha nchi yao kwa ajili ya kukimbilia maisha bora Ulaya, huishia kwenye mikono ya magenge maovu, na wengine hupoteza maisha katika safari hatarishi za baharini.

Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji inaonesha kuwa, Gambia inakabiliwa na matatizo mengi kwani kiwango cha ukosefu wa kazi katika nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika ni asilimia 40.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *