TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imetinga hatua ya 16 bora ya Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) na kuweka rekodi ya aina yake, tangu timu hiyo ianze kushiriki mashindano hayo.
Taifa Stars ilishiriki kwa mara ya kwanza Afcon mwaka 1980, kisha ikashiriki tena mwaka 2019 na mwaka 2023, kabla ya kushiriki mashindano yanayoendelea sasa ikiwa ni mara ya nne.

Pamoja na mara kadhaa kufuzu kucheza mashindano hayo, timu hiyo mara zote imeishia hatua ya makundi na kushindwa kuvuka hatua hiyo.
Stars iko chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Miguel Gamondi aliyepewa timu hiyo muda mfupi kabla ya kuanza kwa mashindano hayo nchini Morocco.
Kwa kweli Morocco ni timu kubwa si tu Afrika, ila duniani baada ya kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia na kuwa timu pekee ya Afrika iliyowahi kufikia hatua hiyo.

Pia, timu hiyo ambayo itacheza dhidi ya Taifa Stars katika hatua hiyo ya 16 bora kesho, ina wachezaji wakubwa wengine wanacheza soka katika timu kubwa Ulaya.
Hayo yote yasiwatie hofu Stars, kikubwa waingie kwa nidhamu wakiiheshimu Morocco na kupunguza kufanya makosa ya kizembe yanayoweza kuigharimu timu kwa mipira iliyokufa, kwani wachezaji wake wengi ni mahiri kutumia mipira hiyo.
Stars ndio muda wake wa kufanya maajabu na kuishangaza Afrika kwa kuwalaza Simba hao wa Milima ya Atlasi, ambao wamekuwa wakifanya makubwa katika soka la Afrika.

Kwanza, tunapenda kuipa hongera Taifa Stars kwa kupenya makundi. Tunaishauri ipunguze makosa ya wachezaji mmojammoja ili tusisababishe penati, kama tulivyosababisha mikwaju hiyo katika mechi mbili za hatua iliyopita.
Pia, tuwakumbushe Watanzania wakati mashindano hayo yakiendelea, hakuna cha kuwadai Taifa Stars hadi sasa kwa kazi waliofanya, pamoja na kufuzu kwa kupitia mshindwa bora baada ya kushika nafasi ya tatu katika kundi.
Hongera tena Stars kwa hilo, kwani mmeweka historia ya kufikia hatua hiyo ambayo haijawahi kufikiwa hata mara moja. Tuwaombee Stars, kila mtu kwa imani yake ili timu hiyo iendelee kuweka rekodi na kudhihirisha ukuaji wa soka la Tanzania.

Na hiyo ni dalili kwamba serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanya makubwa kuhakikisha soka linatembea na kutoa matunda chanya, na hilo lilianzia katika Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) yaliyoandaliwa na Tanzania, Uganda na Kenya.
Watanzania tuwe kitu kimoja tuache mihemko ya Usimba na Uyanga. Wote tuiombee timu hiyo ili iweze kuendelea kufanya maajabu na kusonga mbele.