
Venezuela imelaani “uchokozi mkubwa wa kijeshi” leo Jumamosi baada ya milipuko kutikisa mji mkuu wa nchi hiyo usiku kucha, na Rais Nicolas Maduro kutangaza hali ya hatari.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Venezuela inafutilia mbali, inashtumu, na inalaani (…) uchokozi mkubwa wa kijeshi unaofanywa na (…) Marekani dhidi ya eneo la Venezuela na raia wake, katika maeneo ya kiraia na kijeshi ya Caracas na majimbo ya Miranda, Aragua, na La Guaira yanayozunguka Caracas,” kulingana na taarifa ya serikali. Rais Nicolás Maduro ametangaza hali ya hatari na kutoa wito kwa “vikosi vyote vya kijamii na kisiasa nchini kuzidua mipango ya uhamasishaji,” taarifa hiyo imesema.
Milipuko mikubwa ikiwa ni pamoja na milio inazofanana na ndege zinazoruka juu ya anga ya mji wa Caracas ilisikika karibu saa 2 asubuhi (1 asubuhi saa za Ufaransa) Jumamosi huko Caracas, mji mkuu wa Venezuela, mwandishi wa habari wa AFP ameripoti. Rais Maduro ametangaza hali ya hatari na kutoa wito wa “uhamasishaji.”
Malengo ya kijeshi huenda yamelengwa
Malengo ya kijeshi huenda yamelengwa, ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa kijeshi wa Carlota katikati ya jiji, pamoja na eneo la Fuerte Tiuna, kambi ya kijeshi kusini mwa mji mkuu, anaripoti mwandishi wetu huko Caracas, Alice Campaignolle, ambaye ameona helikopta ikiwaka moto katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Carlota.
Vyanzo visivyojulikana vinathibitisha mashambulizi ya kijeshi kwa vyombo vya habari vya Marekani
Jeshi la Marekani limefanya mfululizo wa mashambulizi mapema Jumamosi dhidi ya mji mkuu wa Venezuela, Caracas, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Marekani. CBS News na Fox News zimewanukuu maafisa wasiotajwa majina kutoka kwa utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump, wakithibitisha kuhusika kwa vikosi vya Marekani. Ikulu ya White House na Pentagon hazijatoa maoni kuhusu milipuko au ripoti za ndege zinazoruka juu ya mji mkuu wa Venezuela.
FAA yapiga marufuku ndege za kibiashara za Marekani kuruka juu ya eneo la Venezuela
Mamlaka ya Anga ya Shirikisho (FAA) imepiga marufuku ndege za kibiashara za Marekani kuruka juu ya anga ya Venezuela katika mwinuko wowote, ikitaja hatari za kiusalama “zinazohusiana na shughuli zinazoendelea za kijeshi.” Uamuzi huu unaanza kutumika kwa saa 23, kuanzia saa 8:00 usiku Jumamosi (saa za Venezuela).
Rais wa Colombia alaani shambulio la “makombora” dhidi ya Caracas
Rais wa Colombia Gustavo Petro amelaani shambulio la “makombora” dhidi ya Caracas siku ya Jumamosi, kufuatia milipuko mikubwa katika mji mkuu wa Venezuela. “Tahadhari kwa ujumla, wameshambulia Venezuela,” ameandika Rais wa Colombia Gustavo Petro, mshirika wa karibu wa Nicolás Maduro, kwenye ukurasa wake wa Twitter. Petro ametaka mkutano wa “haraka” wa Shirika la Mataifa ya Amerika (OAS) na Umoja wa Mataifa ili kutoa uamuzi kuhusu “uhalali wa kimataifa” wa “uchokozi” huu dhidi ya nchi jirani.