Serikali kujenga kiwanda cha chakula cha samaki MwanzaSerikali kujenga kiwanda cha chakula cha samaki Mwanza

SERIKALI imesema kuwa itajenga Kiwanda cha Kutengeneza chakula cha samaki jijini Mwanza kwa lengo la kuwapunguzia gharama wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ili kuongeza uzalishaji wa samaki nchini.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani amesema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na wanufaika wa mradi wa vizimba vya kufugia samaki eneo la Kisoko mkoani Mwanza.

Alisema wizara hiyo imepanga kujenga kiwanda hicho ili kuwapunguzia mzigo Watanzania wenye nia ya kufanya uzalishaji kupitia ufugaji wa samaki.

“Kupitia miradi ambayo tumepata fedha kutoka kwa wadau wetu wa maendeleo, tunakuja kujenga kiwanda kingine sisi kama wizara, kwa ajili ya kutengeneza chakula cha samaki,” alisema Ng’wasi.

Alisema yapo maelekezo mahususi kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuongeza nguvu katika uwekezaji wa uvuvi wa samaki.

Aidha, aliongeza kuwa wizara imeshaandaa mpango wa kukutana na wadau wa sekta binafsi ili kuzungumza nao kwa ajili ya kuzalisha vifaranga vya samaki na vyakula vya samaki vitavyopatikana kwa gharama nafuu kwa manufaa ya wananchi.

“Tunaendelea kutengeneza mpango ambao utatukutanisha sisi na sekta binafsi ili kuweza kuzungumza nao namna bora ya kuwahusisha ili na wao kupitia uwekezaji iwe ni kwa kuzalisha vifaranga vya samaki au kuzalisha vyakula vitakavyokuwa na bei ndogo na rafiki zaidi,” alifafanua.

Ng’wasi pia, alisema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo katika hatua za kuongeza wigo wa mikopo inayotolewa na serikali iguse watu wote wanaohusika na mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *