
Nini kilitokea usiku wa Jumamosi, Januari 3, kuamkia Jumapili, Januari 4, 2026, nchini Burkina Faso? Wafuasi wa utawala wa kijeshi wanabaini kwamba jaribio la mapinduzi lilishindwa. Hata hivyo, katika hatua hii, hakuna taarifa rasmi iliyothibitisha taarifa hii. Tangu siku ya Jumapili, rekodi za sauti zilizowasilishwa kama ushahidi wa njama dhidi ya Kapteni Ibrahim Traoré zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii. Wanajeshi kadhaa wamekamatwa.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Nchini Burkina Faso, kulingana na vyanzo vya usalama, jambo hilo lilikuwa likifuatiliwa kwa karibu na idara za ujasusi kwa wiki kadhaa. Kulingana na wafuasi wa serikali, operesheni hiyo ilipangwa kuanza usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili.
Vyanzo hivi pia vinadai kwamba “mkuu wa kitengo cha ndege zisizo na rubani, pamoja na washirika kadhaa wa karibu wa Ibrahim Traoré, wote wanajeshi na raia,” walikuwa miongoni mwa walengwa waliotajwa na kile wanachokielezea kama “wapangaji njama wanaoungwa mkono na wafadhili wa kigeni.”
“Watu wanaendelea kukamatwa”
Wakati huo huo, “watu wanaendelea kukamatwa,” kinathibitisha chanzo kimoja huko Ouagadougou. Watu mashuhuri katika jumuiya ya wafanyabiashara “wanaweza kuhusishwa na jaribio hili jipya la kuhatarisha usalama ,” chanzo hicho kimeongeza.
Lakini kwa sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa. Kwenye mitandao ya kijamii, kurasa za wawatu wanaomuunga mkono Traoré zimeshiriki mazungumzo ambapo sauti mbili zinaweza kusikika. Kulingana na wafuasi hawa wa serikali, mazungumzo hayo yanamhusu rais wa zamani wa mpito, Luteni Paul-Henri Sandaogo Damiba, ambaye alipinduliwa mnamo mwezi Septemba 2022 na yuko uhamishoni nchini Togo, pamoja na mmoja wa washirika wake wanaodaiwa kuhusika, ambaye bado hajatambuliwa.