DAR ES SALAAM: Klabu ya Singida Black Stars imesema haina pingamizi lolote kwa mamlaka husika endapo Miguel Gamondi atateuliwa kuwa kocha wa kudumu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, nafasi ambayo kwa sasa anaihudumia kwa muda.
Katika mabadiliko ya kiutendaji yaliyotangazwa leo Jumatatu, Januari 5, 2025 na Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Gamondi ameondolewa katika nafasi ya ukocha mkuu wa timu na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Singida Black Stars.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Gamondi katika nafasi yake mpya atakuwa na dhamana ya kusimamia mipango yote ya kiufundi pamoja na maendeleo ya jumla ya timu kwa lengo la kuimarisha ushindani wa klabu hiyo.
Sambamba na mabadiliko hayo, Singida Black Stars imemtangaza David Ouma kuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo.
Kocha Ouma atasaidiwa na makocha wasaidizi Mousa Nd’aw na Muhibu Kanu, huku benchi hilo jipya likitarajiwa kuanza kazi mara moja.
