Nchini Sudan, madaktari wanaonya kuhusu janga la kibinadamu linalokaribia Kordofan Kusini,eneo lililozingirwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), haswa katika mji wa Dilling, ambao umekumbwa na mashambulizi makali na kizuizi cha muda mrefu.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na shirika la Madaktari wa Sudan, karibu watu milioni mbili wanaishi katika eneo hilo, wakiwemo zaidi ya watu 270,000 waliokimbia makazi yao. Shirika hilo linaogopa kutokea kwa janga lililotokea El-Fasher mwezi Oktoba mwaka uliyopita, ambapo maelfu ya raia waliuawa.

Nchini Sudan, mapigano yameongezeka Kordofan. Baada ya Kordofan Kaskazini, wanajeshi wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), wakiongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Daglo, pia anayejulikana kama Hemetti, sasa waelekeza mashambulizi yao dhidi ya Dilling, katikati ya Kordofan Kusini, eneo la kimkakati lenye idadi ya watu zaidi ya milioni mbili, lililoko kwenye makutano ya barabara kuu zenye shughuli nyingi za biashara kuelekea Chad na Sudan Kusini.

“Kwa mtazamo wa kijeshi, ni eneo la kimkakati, karibu na nchi ambapo RSF inaweza kupata usaidizi kwa urahisi zaidi kuliko katikati ya nchi,” anaeleza Mohamed Faisal Hassan, msemaji wa shirika la Madaktari wa Sudan. “Pia ni eneo linalozalisha mafuta. Viwanda vikuu vya kusafisha mafuta nchini vinapatikana katika eneo hili na Kordofan Magharibi.”

Kwa muhtasari wa kile kinachoendelea Dilling, ni karibu hali ile ile tuliyoiona El Fasher, ambayo ilisababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu katika maeneo yenye watu wengi. Kwa hivyo watu wanateseka sana; tuna viwango vya juu sana vya utapiamlo, haswa miongoni mwa watoto. Ni mgogoro wa kweli sasa.

“Hali kama ile ya El-Fasher”

Kulingana na Umoja wa Mataifa, hali ya kibinadamu huko Dilling, kama ilivyo Kadugli, mji mkuu wa Kordofan Kusini, ambao umekuwa ukizingirwa kwa wiki kadhaa, inazidi kuwa mbaya. Akiba ya chakula na dawa inapungua, na bei ya mahitaji ya msingi imeongezeka mara tano, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA).

Vifo vya kila siku vinaripotiwa, na utapiamlo mkali unaongezeka, haswa miongoni mwa watu waliokimbia makazi yao. shirika la kimataifa la Human Rights Watch pia linaripoti kwamba mashambulizi  ya RSF hulenga miundombinu ya raia mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na hospitali na shule.

Kulingana na madaktari wa Sudan, zaidi ya watu 200,000 kwa sasa wamenaswa Dilling na Kadugli, bila ufikiaji salama wa misaada ya kibinadamu. “Raia hawapaswi kamwe kuwa sehemu ya usawa katika vita hivi,” analaani Mohamed Faisal Hassan.

“Waathiriwa wa kwanza watakuwa watoto, vijana, wanawake wajawazito, na kadhalika. Ni hali ile ile tuliyoiona El Fasher. Wanafanya hivi ili kuwalazimisha watu kukimbia mji.”

Madaktari wa Sudan wanatoa wito wa kuondolewa mara moja kwa mzingiro dhidi ya Dilling na Kadugli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *