Rais Trump ametishia kuishambulia Venezuela kwa mara ya pili iwapo “hawatobadilisha mwenendo,” huku pia akitishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya serikali ya Colombia.
Akizungumza na waandishi wa habari, alisema kuwa operesheni kama hiyo “inaonekana kuwa wazo zuri kwake.”
“Tunakabiliana na watu ambao ndiyo kwanza wameapishwa madarakani. Msiniulize ni nani aliye madarakani kwa sababu nitatoa jibu litakalokuwa na utata mkubwa,” Trump aliwaambia waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya Air Force One, alipoulizwa kama amezungumza na kiongozi wa mpito Delcy Rodriguez.
Aliposisitizwa kueleza alichomaanisha, Trump alisema: “Hii ina maana kwamba sisi ndiyo tuko madarakani.”
Wakati huo huo, Delcy Rodriguez siku ya Jumapili alitoa wito wa kuwepo kwa uhusiano wa “usawa na wa heshima” kati ya Venezuela na Marekani, siku moja baada ya majeshi ya Marekani kuishambulia Caracas na kumkamata kiongozi wa mrengo wa kushoto, Nicolas Maduro.
“Tunaona kuwa ni kipaumbele kusonga mbele kuelekea uhusiano wa usawa na wa heshima kati ya Marekani na Venezuela,” Rodriguez, ambaye ni makamu wa rais wa Maduro, aliandika kwenye Telegram.
“Tunaialika serikali ya Marekani kushirikiana nasi katika ajenda ya ushirikiano inayolenga maendeleo ya pamoja.”
Trump: Operesheni nchini Colombia “inaonekana kuwa wazo zuri”
Akizungumzia Colombia, Trump alisema nchi hiyo inaendeshwa na “mtu mgonjwa,” na akasema operesheni ya kijeshi huko “inaonekana kuwa wazo zuri.”
“Colombia nayo ina matatizo, inaendeshwa na mtu mgonjwa, anayependa kutengeneza kokeini na kuiuza Marekani, na hataendelea kufanya hivyo kwa muda mrefu,” Trump aliwaambia waandishi wa habari, akionekana kumuashiria Rais wa Colombia, Gustavo Petro.
Alipoulizwa moja kwa moja kama Marekani ingefanya operesheni ya kijeshi dhidi ya Colombia, Trump alijibu: “Inaonekana kuwa wazo zuri kwangu.”