MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Ahmed Abbas amewaagiza wakuu wa wilaya zote katika mkoa huo kuwachukulia hatua wazazi watakaoshindwa kupeleka watoto shule kupata elimu. Agizo hilo amelitoa nyakati katika ziara yake kukagua ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwemo ya vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na miundombinu mingine wilayani Songea.
Amesema serikali imetimiza wajibu wake kuhakikisha miundombinu ya elimu ipo na walimu wapo, hivyo jukumu pekee lililobaki ni wazazi kuhakikisha wanapeleka watoto wao shule kupata haki yao ya msingi.Abbas alisema serikali haitakuwa na huruma kwa mzazi au mlezi atakayeshindwa kupeleka mtoto wake shule na kuwataka viongozi kuanzia ngazi ya vijiji hadi wilayani kusimamia kwa karibu mahudhurio ya watoto hao katika maeneo yao.
“Nawataka wakuu wa wilaya na watendaji wengine walio chini kwenye maeneo yao,” akaongeza , “Hakikisha watoto wote wenye sifa na wanaotakiwa kuanza elimu ya awali, msingi na wale waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza katika muhula wa masomo 2026 wanaripoti katika shule walizopangiwa tarehe 13 mwezi huu”.
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Ruvuma, Edith Mpinzile alisema mpango wa mkoa huo ni kuanza masomo rasmi Januari 13, 2026, hivyo wanafunzi wote waliopangiwa kujiunga na kidato cha kwanza na shule za msingi wanapaswa kufika shuleni kuanza masomo. Mpinzile alisema wanafunzi wa darasa la awali walioandikishwa watapokewa ili kuhakikisha nao wanapata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.
Amewaagiza walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu wa shule za sekondari mkoani humo kutowarudisha nyumbani watoto ambao hawana sare za shule kwani jukumu hilo ni la wazazi na si watoto. Kwa mujibu wa Mpenzile, walimu wakuu na viongozi wa shule kupitia kamati za shule hawana budi kusoma na kufuata miongozo ya elimu na kutoa uelewa sahihi kwa wazazi na walezi ili kuondoa mkanganyiko.
Mzazi na mkazi wa Bombambili katika Manispaa ya Songea, Ali Mselem amesema Mkoa wa Ruvuma umekuwa ukifanya vibaya kielimu hali inayosababishwa kwa baadhi ya walimu kutotimiza wajibu wao ipasavyo. Mselem amesema badala ya kufundisha watoto darasani, baadhi ya walimu wamekuwa wakijikita zaidi katika shughuli za kujiongezea mapato. Mkazi mwingine, John Ndumbaro ameshauri serikali kuongeza motisha na mishahara ya walimu kama njia ya kurudisha hali na morali ya ufundishaji.
Ameongezea kuwa wapo baadhi ya walimu wanaoweka nguvu kubwa kufundisha masomo ya ziada kwa baadhi ya watoto kuliko wanavyofundisha katika madarasa ya kawaida ili kujiongezea mapato. SOMA: SUA yazindua mitaala mipya masomo elimu ya amali
