WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera ametangaza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuchukua hatua za kuwapelekea wananchi Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Samia kwenye ngazi ya wilaya ikilenga kuwaondolea migogoro inayowakabili hususani inayohitaji usaidizi wa kisheria.
Akiwa mkoani Morogoro ambako programu hiyo ilifanyika mwaka jana kama ilivyokuwa kwa mikoa mingine, Dk Homera amesema bado kuna uhitaji mkubwa wa wananchi kupata huduma hiyo ili kuondoa changamoto zinazowakabili.
Kutokana na hilo, amesema wizara iko kwenye maandalizi ya kupeleka huduma hiyo kwa kila wilaya kwa nchi nzima kwani jukumu lao ni kuwafuata wananchi kuwasogezea huduma ya msaada wa kisheria ili wanufaike na serikali yao.
Kampeni imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususani katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla.
Kwa mujibu wa wizara, lengo kuu la kampeni ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.
Katika kufikia lengo hilo, kampeni inaongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususani haki za wanawake na watoto; inatoa huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia; kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu elimu ya sheria, masuala ya haki na wajibu na misingi ya utawala bora.
Uamuzi huu wa serikali ni habari njema kwa sababu wakati programu ilipoendeshwa mwaka jana yalikuwapo matokeo makubwa kwani iliwezesha kutatua migogoro mingi ya wananchi waliofikiwa na huduma hii muhimu.
Takwimu zinaonesha wananchi zaidi ya milioni 40 walifikiwa na kampeni hiyo na kusikiliza milioni ya kero ambazo zilijikita katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya mirathi, ndoa, ardhi, haki za binadamu, unyanyasaji wa kijinsia, masuala ya watoto na haki za makundi, miongoni mwa kero hizo.
Kama hiyo haitoshi, wizara ilieleza imeweka mikakati na mipango endelevu ikiwamo kuanzisha madawati ya msaada wa kisheria kwa kila halmashauri ambako kutakuwa na maofisa maendeleo ya jamii watakaohusika kutoa msaada huo.
Kwa kutazama mafanikio ya kampeni hii mwaka jana pamoja na mikakati hii ya serikali, sisi tunaona dhahiri nia njema ya serikali kuendelea na kampeni hii kwani mahitaji ya wananchi kuhusu masuala ya msaada wa kisheria ni makubwa.
Tunaamini hatua zote hizi zinazochukuliwa zinalenga kuwaondolea migogoro wananchi na zaidi kufikia matokeo ya muda mrefu ya kampeni hii ambayo ni kuchangia katika kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza hususani wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi.
Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kisiasa nchini.
