Mkasa wa moto wazusha taharuki huku Berlin ikikosa umemeMkasa wa moto wazusha taharuki huku Berlin ikikosa umeme

Shambulio hilo la uchomaji lililotokea katika eneo la kusini-magharibi mwa Berlin lenye miti mingi, lilisababisha kukatika kwa umeme kwa takribani kaya 45,000, hali iliyoathiri pia huduma za treni za ndani, shule, maduka na hata hospitali. Wakazi wengi walijikuta bila umeme na joto majumbani wakati theluji ikiendelea kushuka.

Mkazi wa eneo hilo, Jutta Herter mwenye umri wa miaka 77, amesema amekasirishwa sana na tukio hilo. Akiwa nyumbani pamoja na mume wake, walilazimika kuwasha moto chumbani ili kupata joto, lakini hali hiyo iliongeza kiwango cha joto hadi nyuzi joto 13 pekee.

Katika ukumbi wa manispaa wa Zehlendorf, wakazi kadhaa walikusanyika kutafuta joto, vinywaji vya moto na umeme wa kuchaji simu na vifaa vingine. Wengi wao walihofia kuondoka nyumbani kwa muda mrefu kwa kuhofia mabomba ya maji kuganda kutokana na baridi kali. Herter alihoji nia na utu wa waliohusika na shambulio hilo, akisema tukio hilo halieleweki kabisa.

Ujerumani Berlin 2026 | Wanafunzi katika makazi ya dharura baada ya shambulio la uchomaji moto na kukatika kwa umeme
Wanafunzi katika makazi ya dharura baada ya shambulio la uchomaji moto na kukatika kwa umemePicha: Omer Messinger/AFP/Getty Images

Kundi moja ladai kuhusika

Kundi linalojiita Vulkangruppe, limedai mtandaoni kuhusika na shambulio hilo, likisema linalenga kile walichokiita uchumi wa nishati ya mafuta unaochochea mabadiliko ya tabianchi. Tukio hilo linafuatia shambulio jingine lililotokea Septemba mwaka jana, ambapo nguzo za umeme zilichomwa na kusababisha giza katika maeneo ya kusini-mashariki mwa Berlin.

Idara ya ujasusi wa ndani nchini Ujerumani inaendelea kuchunguza iwapo madai ya kundi hilo ni ya kweli. Wakati huohuo, baadhi ya wanasiasa wa upinzani wameibua wasiwasi juu ya uwezekano wa kuhusika kwa Urusi, hasa ikizingatiwa madai ya Ujerumanikuhusu mashambulizi ya kile kinachoitwa vita mseto, ikiwemo ujasusi na upotoshaji wa taarifa mtandaoni.

Mbunge wa chama cha kihafidhina cha CDU, Roderich Kiesewetter, amesema lolote linawezekana, akidai kwamba tamko la kundi hilo linaonekana kuwa limeandikwa kwa Kirusi kisha kutafsiriwa vibaya kwa Kijerumani.

Msaada wa kwa wahanga

Wakati huo huo, idara ya huduma za dharura ya Berlin, kwa kushirikiana na jeshi na mashirika ya misaada, imekuwa ikisaidia wakazi walioathirika katika wilaya ya Steglitz-Zehlendorf. Wakazi wa nyumba za wazee wamehamishwa kwenda maeneo yenye joto, huku hoteli, shule na vituo vya michezo vikigeuzwa kuwa makazi ya muda.

Tamasha la Taa Berlin laendelea licha ya mzozo wa nishati

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Hadi kufikia mchana wa Jumatatu, kaya zipatazo 14,500 zilikuwa zimerejeshewa umeme, ingawa mamlaka zinasema umeme hautarejea kikamilifu hadi Alhamisi.

Mkazi mwingine, Philipp Pasemann mwenye umri wa miaka 32, amesema hali ni baridi na giza, lakini anaendelea kuvumilia kwa kutumia blanketi na mishumaa.

Akizungumzia tukio hilo, Meya wa Berlin, Kai Wegner, amesema shambulio hilo limeonyesha kwa mara nyingine udhaifu wa miundombinu muhimu ya nchi. Naye mwenyekiti wa kamati ya bunge inayosimamia vyombo vya ujasusi, Marc Henrichmann, ameahidi kuwa serikali itafanya kila iwezalo kupambana na itikadi kali za vurugu na maadui wa demokrasia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *