KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu, amewataka wananchi ambao bado hawajachukua Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kufika katika Ofisi za Wilaya za mamlaka hiyo ili kuvichukua, akisisitiza kuwa ni nyaraka muhimu ya utambulisho ambayo serikali imetumia gharama kubwa kuizalisha.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Gugu alisema kila Mtanzania anatakiwa kumiliki kitambulisho cha Taifa kwa kuwa ni nyaraka rasmi inayotambulika kisheria na hutumika katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Amesema mamlaka pia imeanzisha short code ya bure itakayowawezesha wananchi kupata mrejesho wa huduma za vitambulisho kupitia simu za mkononi bila malipo, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa taarifa hasa kwa wananchi wa vijijini.
“Tunaamini huduma hii itawasaidia wananchi wengi kufuatilia hatua mbalimbali za usajili na kujua taarifa zao wakiwa katika maeneo yao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufika ofisini,” alisema. SOMA: Namba ya NIDA sasa kupatikana kwa ujumbe mfupi

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema zaidi ya vitambulisho 300,000 bado havijachukuliwa katika ofisi za wilaya nchini na amewasihi wananchi kujitokeza kuvichukua kwa wakati. “Kuna idadi kubwa ya vitambulisho viko ofisini, tunawaomba wananchi wafike kuvichukua kwani Serikali imetumia fedha nyingi kuvizalisha,” alisema Kaji. Aidha, amewataka wananchi wenye makosa kwenye taarifa zao kutumia fursa ya kibali maalumu cha kufanya marekebisho kabla ya muda wa mwaka mmoja wa kibali hicho kuisha.