Salah alifunga bao la ushindi katika dakika za nyongeza na kuipeleka Misri kwenye robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Benin katika mechi iliyochezwa Agadir.
Nahodha huyo wa Misri alifunga dakika ya 124, akihitimisha ushindi muhimu kwa timu yake. Licha ya Misri kuwa bingwa wa AFCON mara saba—rekodi barani Afrika—mara ya mwisho kutwaa taji hilo ilikuwa mwaka 2010, na Salah bado hajawahi kulishinda kombe hilo.
Misri ilipata bao la kwanza dakika ya 69 kupitia Marwan Attia aliyemalizia pasi safi ya Mohamed Hany. Benin, ambao wako nafasi 92, Misri nafasi ya 35 katika viwango vya FIFA, walilazimisha muda wa nyongeza baada ya Jodel Dossou kusawazisha dakika ya 83.
Katika muda wa nyongeza, Yasser Ibrahim aliirejesha Misri mbele kwa bao la kichwa dakika ya saba ya kipindi hicho, kabla ya Salah kufunga bao la tatu mwishoni kabisa na kuondoa shaka yoyote kuhusu matokeo. Bao hilo lilikuwa la tatu kwa Salah katika mashindano haya.
Misri sasa itasalia Agadir kusubiri mshindi kati ya Ivory Coast na Burkina Faso katika robo fainali.
Akizungumza baada ya mechi, kocha wa Misri Hossam Hassan alisema:
“Nilisema kabla ya mechi kuwa hakuna timu ndogo. Benin walikuwa wagumu. Misri ni timu kubwa na nataka kuwafurahisha watu wangu.”
Super Eagles waonyesha ubabe
Nigeria ilitoa onyesho la nguvu baada ya kuichapa Msumbiji 4-0 katika mechi iliyochezwa chini ya mvua kubwa mjini Fes. Victor Osimhen alifunga mabao mawili huku Ademola Lookman akihusika katika mabao yote manne.
Lookman alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 20 kwa kumalizia pasi ya Akor Adams. Osimhen aliongeza bao la pili dakika ya 25 baada ya krosi ya Lookman kugonga Adams kabla ya kumfikia.
Mshambuliaji huyo wa Galatasaray alifunga tena muda mfupi baada ya kipindi cha pili kuanza, likiwa bao lake la tatu katika mechi tatu za AFCON, baada ya kushindwa kufunga katika mechi zake saba za awali za mashindano hayo.
Lookman aliendelea kung’ara kwa kutoa pasi ya nne iliyomkuta Adams aliyefunga dakika 15 kabla ya mchezo kumalizika, na kuipa Nigeria ushindi wake mkubwa zaidi katika hatua ya mtoano ya AFCON tangu Misri ilipoifunga Algeria 4-0 mwaka 2010.
Nina furaha sana. Timu imecheza vizuri na kufunga mabao manne. Tunatumaini kuendelea na kiwango hiki, alisema Lookman.
Licha ya kutolewa, Msumbiji wanaondoka kifua mbele baada ya kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Nigeria sasa inaelekea Marrakesh kwa robo fainali itakayochezwa Jumamosi dhidi ya mshindi kati ya Algeria na DR Congo. Timu hizo zitakutana Rabat Jumanne, ambapo ushindi wa DR Congo unaweza kuwapa Nigeria nafasi ya kulipiza kisasi baada ya kupoteza kwao kwa mikwaju ya penalti katika mchujo wa Kombe la Dunia mwezi Novemba.
Mechi za mwisho za hatua ya 16 bora zitachezwa Jumanne (06.01.2026), ambapo Algeria itachuana na DR Congo kabla ya Ivory Coast kuvaana na Burkina Faso mjini Marrakesh.