Mazungumzo hayo yanafanyika baada ya siku kadhaa za mapigano kati ya vikosi vyake vinavyoungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na wapinzani wanaoungwa mkono na Saudi Arabia.

Mazungumzo hayo yanayoandaliwa na Saudi Arabiayanaashiria kuanza kwa jitihada za kupunguza mvutano baada ya mapigano katika maeneo yanayoongozwa na serikali ya Yemen, ambayo yalionyesha mpasuko kati ya mataifa ya Ghuba — Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

“Ujumbe mkubwa ukiongozwa na rais wa Baraza la Mpito la Kusini (STC), Aidaros Alzubidi, utasafiri kwenda Riyadh jioni ya leo(06.01.2026) kwa mwaliko rasmi wa Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia, Prince Khalid bin Salman,” alisema afisa mmoja wa STC akiomba jina lake lisitajwe kutokana na unyeti wa mazungumzo hayo.

Alzubidi pia atajadili “mazungumzo ya kusini yanayodhaminiwa na Riyadh,” afisa huyo aliongeza.

Saudi Arabia ilizihimza pande zote za Yemen kufanya mazungumzo mjini Riyadh kufuatia ombi la serikali ya Yemen, na pande zote zimekubali kushiriki.

Yemen Seiyun 2026 | Mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vya STC kusini mwa nchi
Mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vya STC kusini mwa nchiPicha: Aden Independent Channel (AIC TV)/AFP

Mwezi Desemba, wapinzani wanaoungwa mkono na UAE waliteka maeneo makubwa, ikiwemo sehemu kubwa ya jimbo la Hadramawt linalopakana na Saudi Arabia, na kuwafukuza wanajeshi wa serikali wanaoungwa mkono na Saudi Arabia.

Lakini wiki iliyopita, mashambulizi ya anga kutoka muungano unaoongozwa na Saudi Arabia na mashambulizi ya ardhini yalifanikiwa kuwazuia wale wanaotaka kujitenga.

Saudi Arabia na UAE, ambazo zote ni mataifa tajiri ya mafuta na jirani, kwa muda mrefu zimekuwa zikiunga mkono makundi hasimu ndani ya serikali yenye mgawanyiko ya Yemen iliyoko kusini mwa nchi.

Hapo awali waliungana katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran, ambao waliiondoa serikali madarakani mwaka 2014 na kuchukua maeneo mengi ya kaskazini mwa Yemen.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *