Mataifa mbali mbali ya ulimwengu yameendelea kulaani hatua ya Marekani ya kumteka, kumpeleka na kumfungulia mashtaka nchini Marekani, kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro.
Kikao cha dharura cha baraza la usalama jana kimesisitiza juu ya kuheshimiwa sheria za kimataifa, huku kiongozi wa upinzani wa Venezuela, Maria Corina Machado akimsifia rais Donald Trump kwa kumkamata Maduro.
Maria Corina Machado amezungumza jana Jumatatu na kituo cha habari cha Fox ambako aliitaja tarehe tatu Januari kama siku inayooingia kwenye vitabu vya historia, haki ilipotendeka na udhalimu kushindwa.
Vikosi vya Marekani vilishambulia Venezuela na kumteka Maduro na mkewe Cilia Flores na kumsafirisha hadi Newyork ambako jana walifunguliwa mashataka ya tuhuma za usafirishaji madawa ya kulevya.
Machado ameeita hatua hiyo ya Marekani kuwa muhino sio tu kwa Wavenezuela bali hata kwa ubinadamu,uhuru na heshima ya utu.
Viongozi mbali mbali wa ulimwengu lakini wameendelea kutilia mashaka hatua ya Marekani-Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumzia wasiwasi wake kuhusu ukosefu wa uthabiti ndani ya Venezuela, wakati baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likisisitiza juu ya kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa huku pia likiwa na wasiwasi wa kitakachoendelea Venezuela. Venezuela
Rosemary Dicarlo naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kisiasa alikuwa na haya.
“Nina wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kuongezeka ukosefu wa usalama nchini Venezuela, uwezekano wa kusababisha athari mbaya kwenye kanda nzima na mtazamo unaoweza kujengeka kuhusu mahusiano miongoni mwa mataifa, jinsi yanavyotakiwa kuendeshwa”
DiCarlo ameliambia baraza la usalama kwamba, kuidumisha amani ya kimataifa na usalama kutategemea kuendelezwa kwa ahadi za wanachama wote za kuheshimu mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Washirika na wasiokuwa washirika wa Marekani wametumia mkutano huo wa baraza la usalama la usalama la Umoja wa Mataifa kuikosoa Marekani.
Rais Donald Trump anashikilia kwamba hatua yake anayooita ”Kumkamata” Maduro haijavunja sheria. Wachambuzi wa siasa na viongozi mbali mbali wa Ulimwengu kuanzia China, Colombia hadi Mexico wameilaani operesheni hiyo dhidi ya Venezuela huku ukiweko wasiwasi wa kitakachofuata.Maduro ajitetea mahakamani baada ya kukamatwa na Marekani
Ndani ya Venezuela kwenyewe imeripotiwa jana Jumatatu kwamba milio ya risasi ilisikika mfululizo karibu na makaazi ya rais, polisi wakichukua hatua kudhibiti droni zilizokuwa zinaruka kwenye eneo hilo bila ya kibali.
Sauti ya miripuko pia ilisikika mjini Caracas huku watu wakihamishwa kutoka majengo ya serikali kufuatia tukio hilo. Wizara ya mawasiliano ya Venezuela ilisema hakuna makabiliano ya risasi au vurugu zilizoripotiwa kwenye eneo hilo na hali hivi sasa kwa ujumla, nchi nzima ni tulivu.