Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan anasema kufikiwa kwa amani ya kudumu katika vita vya Urusi na Ukraine sasa “kuko karibu”.

“Kwa maoni yangu, baada ya miaka minne ya vita, sasa hivi tuko karibu kufikia amani ya kudumu. Kwa uchache, tunaona maeneo kadhaa ambayo ni muhimu kwa upatikanaji wa amani yanajadiliwa kwa uzito zaidi,” Fidan amewaambia waandishi wa habari katika Ubalozi wa Uturuki mjini Paris siku ya Jumanne baada ya mkutano wa Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu Ukraine.

Akisisitiza kuhusu umuhimu wa mkutano wa Paris, Fidan alisema alimwakilisha Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mkutano huo, ambao pia ulihudhuriwa na viongozi wa mataifa na taasisi kama vile EU na NATO. “Masuala muhimu yalijadiliwa,” alisema.

“Tunachokiona ni kuwa, yakitiwa saini, haya hayatokuwa makubaliano tu ya amani yatakayomaliza vita nchini Ukraine. Yatatoa muelekeo ya muda mrefu, ya namna amani itakavyokuwa kati ya Urusi na Ulaya kwa ujumla. Wakati huo huo, yatakuwa ya masuala kadhaa ambayo yataangazia sera ya Urusi katika kanda,” waziri huyo wa mambo ya nje wa Uturuki aliongeza.

‘Ni suala la msingi kwa Uturuki kuwa na jukumu la usalama katika Bahari Nyeusi’

Fidan alisema uwezekano wa kusitishwa mapigano, kuzuia Ukraine, na uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi pale usitishwaji wa mapigano utakapokiukwa yalikuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa.

“Kuanzia mwanzo, chini ya maagizo ya rais wetu, jeshi letu limekuwa na msimamo kuwa litakuwa na jukumu la ulinzi wa baharini pale amani itakapopatikana. Naamini hatua za msingi zimepigwa kuhusu hili.

“Ukizingatia kuwa Uturuki ni mwanachama wa NATO aliye na idadi kubwa ya vyombo katika Bahari Nyeusi, ni suala la msingi kwa Uturuki kuwa na jukumu la Usalama katika Bahari Nyeusi … Ni matarajio yetu, kuwa makubaliano ya amani yatatiwa saini hivi karibuni, ili kuepusha vifo zaidi na kuleta usalama katika kanda hiyo,” alieleza zaidi.

Fidan alisema kuwa katika kikao kingine siku ya Jumanne kiliangazia kufufua uchumi wa Ukraine iwapo makubaliano ya amani yatatiwa saini.

Alisisitiza kuhusu umuhimu aliouweka Rais Erdogan kuhusu suala hilo na kusema kuwa hakuna nchi “yenye uwezo zaidi ya Uturuki linapokuja suala la kuponya vidonda.”

“Tuko vizuri katika uponyaji wa vidonda na kwa wale watu wanaohitaji misaada. Uwekezaji wa kiuchumi na utaalamu wa wafanyabiashara wetu, hasa katika miundombinu, ni muhimu sana. Tunaamini pindi amani itakapopatikana, Uturuki itakuwa na jukumu muhimu la kufufua uchumi na maendeleo,” aliongeza.

Fidan alisema pia alikuwa na mikutano na wakuu wa nchi, kujadili masuala muhimu, na kufanya tathmini ya kuhusu agenda hiyo na maafisa wa Umoja wa Ulaya.

Mashambulizi ya Israel nchini Syria ‘ni uchokozi’

Fidan aliongeza kuwa pia walijadili masuala kadhaa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Asaad al Shaibani, ambaye alikuwepo Paris kwa mkutano mwingine wa utatu pamoja na Marekani na Israel. Aliongeza kuwa Uturuki inaendelea kufuatilia mazungumzo ya pande hizo tatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *