SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza nguvu nyingi katika elimu inayojenga umahiri, ujuzi na maadili ili kuwaandaa vijana wenye uwezo wa kifi kra, kubuni na kufanya kazi kwa vitendo.
Katika kufanikisha hilo, serikali imechukua hatua kubwa za kufanikisha hilo, mojawapo likiwa kupitia Sera ya Elimu nchini na pia kufanya mapitio ya mitaala ya masomo kwa nia ya kuja na masomo yanayozingatia kufikia elimu ujuzi na umahiri.
Tumeshuhudia mabadiliko hayo ya Sera ya Elimu na pia kuwapo mitaala mipya, vyote vikiwa vimeanza kufanya kazi katika hatua mbalimbali, jambo linalothibitisha utayari wa serikali kuwajengea maarifa mapya vijana wa Kitanzania.
Tumeona msisitizo wa maono hayo kwa Rais Samia kila alipopata fursa ya kuzungumzia sekta ya elimu nchini, au masuala ya vijana na maendeleo pamoja na mikakati ya kuwawezesha vijana na kukuza sekta ya elimu nchini.
Uwekezaji huu una manufaa makubwa kwa sababu yanayofanyika si kwa nia ya vijana kufaulu mitihani yao ya darasani, la hasha! Bali ni kuwaandaa kukabiliana na maisha, soko la ajira na kutoa mchango wao katika maendeleo ya taifa.
Kutokana na umuhimu wake, kuna umuhimu wa vijana wenyewe, wazazi na walezi pamoja na walimu, kufahamu mwelekeo huu wa serikali na kuwa sehemu ya kuchangia mafanikio yake ambayo mwisho wa siku yatakuwa ni taifa zima.
Tunasema hivyo kwa sababu msingi huu wa elimu ujuzi na umahiri ukieleweka vyema na wadau wakiwamo hao tuliowataja, ina maana utekelezaji wake utakuwa rahisi na utatupeleka kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali.
Kwa msingi huo, tunaungana na kauli aliyoitoa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba wiki hii mjini Unguja, ya wananchi, walimu na wanafunzi kwa pamoja waweke kipaumbele katika kulinda, kutunza na kutumia ipasavyo miundombinu ya elimu iliyowekezwa kwa gharama kubwa ambayo ni sehemu ya mradi huu mkubwa.
Miundombinu hii imejengwa kwa gharama kubwa na ni ya kisasa kwa sababu ili kufikia elimu ujuzi na umahiri lazima uwe na shule zenye miundombinu ya kisasa ikiwamo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), inayoakisi malengo hayo ya kuwaandaa vijana kumudu maisha ya ushindani yenye kuongozwa na Tehama.
Dunia inabadilika kwa kasi sana kutokana na maendeleo hayo ya teknolojia, hivyo vijana wanapaswa kutumia nafasi hii ya uwekezaji wa serikali kujiona ni wenye bahati na kuitumia kwa manufaa yao ili kesho yao iwe njema zaidi.
Na katika hili ni lazima wao wenyewe wawe vinara wa mabadiliko, walio tayari kupokea maono hayo ya Rais Samia na serikali yake katika kuwapa elimu ujuzi na umahiri ili Tanzania isibaki nyuma, izalishe wataalamu wengi zaidi wanaoweza kushindana katika soko la ajira lakini watakaiojenga nchi yao.
