MOROGORO: HALMASHAURI ya Wilaya ya Morogoro inatarajia kutoa vyandarua bila malipo kwa kila kaya ili kukabiliana na ugonjwa wa malaria.
Hatua hiyo ni mwanzo wa kuhamasisha kampeni ya utokomezaji wa malaria.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Dk Gosbert Kalunde amesema hayo wakati wa utoaji wa elimu juu ya uzinduzi wa kampeni ya afua ya utoaji wa vyandarua kwa kila kaya za halmashauri hiyo.

Amesema kwa kampeni hiyo inasimamiwa na Mpango wa Taifa wa Kuthibiti wa Malaria kwa kutekeleza afua ya ugawaji wa vyandarua kwa kila kaya zilizopo katika halmashauri hiyo ambayo kitakwimu za kimkoa inaongoza kwa maabukizi.
“Utekelezaji wa afua ya ugawaji wa vyandarua ni kwa kila kaya moja kwa watu wawili watapokea chandarua kimoja na zoezi hili linaanza mwezi huu wa Januari 2026,” amesema Dk Kalunde.
Dk Kalunde amesema kwa kuwa halmashauri hiyo ina ongezeko kubwa la maambukizi ya malaria kwani kati ya watu 100, takribani watu 26 wanakutwa wakiwa na maabukuzi ya malaria.
“…Hivyo afua hii ya matumizi ya vyandarua yanakwenda kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria,”amesema Dk Kalunde.

Dk Kalunde ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuandikisha kaya zao ili zoezi la ugawaji wa vyandarua utakapokuja kuanza utekelezaji wake wajitokeza pia kupikea vyandarua hivyo .
“Lengo letu kuwa asitokee mwananchi akakosa chandarua kwani kila kaya itapata vyandarua tofauti na hapo awali zilikuwa zinatolewa kwa akina mama wajawazito na pia kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano wanapewa wanapokwenda kupata chanjo ya surua inayotolewa kipindi cha miezi tisa,”amesisitiza Dk Kalunde.
Dk Kalunde ametoa wito kuwa vyandarua hiyo wavitumie na waondokane na kasumba ya kwamba vimekuwa na dawa inayosababisha kupunguza uwezo wa nguvu za kiume kwa kuwa jambo hilo halina ukweli kisanyansi.

“Hizo ni imani na ninasisitiza watu wasizifuate bali wachukue hatua ya kutumia vyandarua watakavyopewa ili kujikinga na malaria,”amesema Dk Kalunde.
Amesema watu wasizitumie kwa shughui za kuvulia samaki au kukinga wadudu waharibifu kwenye bustani za mboga bali wazitumie vizuri ili ziweze kuwakinga na ile thamani ya fedha iweze kuonekana.
“Serikali ya awamu ya sita imetoa vyandarua hivi ili kila Mwananchi aweze kuzipata kwa ajili ya kujikinga maambukizi ya malaria,” amesema Dk Kalunde.
Naye Mratibu wa Ugawaji wa Vyandarua Ngazi ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Peter Gitanya amesema halmashauri hiyo inaongoza kwa maabukizi ya malaria na imetengewa vyandarua 231,644.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amewataka watendaji wa ngazi ya vijiji na vitongoji kusimamia vyema zoezi la uandikishaji wa kaya kwa kuhakikisha zote zinaorodheshwa ili kupaya vyandarua hivyo.