Na Emmanuel Oduor

Baada ya Marekani kumteka nyara Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, na kuahidi kuhamasisha makampuni ya nishati ya Marekani kunufaika na utajiri wa mafuta wa nchi hiyo, wasiwasi umeongezeka kuhusu hatua ambazo Marekani inaweza kuchukua katika migogoro na mataifa ya Afrika.

Wataalamu wanasema kuwa hatua hiyo ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela inaweza kuwa ni mfano hatari wa mashambulizi dhidi ya viongozi wa mataifa mengine ambayo yamekuwa na migogoro na serikali ya Rais Donald Trump.

Mataifa ya Afrika pamoja na mashirika ya kikanda barani humo yameshtumu operesheni hiyo ya kushtukiza dhidi ya rais wa Venezuela — ambaye mawasiliano yake ya mwisho hadharani na kiongozi wa Afrika yalikuwa mkutano na Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traore, mjini Moscow wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ushindi ya Urusi mnamo Mei 2025.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alieleza hatua ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela kama onyo kwa Waafrika kuyapa kipaumbele masuala ya usalama wa kimkakati ili kulinda bara lao ardhini, baharini, na ulinzi wa angani. Aliwaonya viongozi wa Afrika dhidi ya kutaka kubaki kuwa “samaki wakubwa kwenye mabwawa madogo”.

“Watu wengine hupenda hali hiyo ya kuwa samaki mkubwa kwenye bwawa dogo. Unajiona mkubwa sana, lakini matatizo yakitokea, huenda usiokoke,” alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari alipoulizwa kuhusu mafunzo ambayo Afrika inaweza kujifunza kutokana na yaliyojiri Venezuela.

Trump tayari amekuwa akiishambulia Nigeria kwa madai yasiyo na msingi ya “mauaji ya Wakristo” na kuitaja kama “Nchi yenye kumtia wasiwasi”. Mwezi uliopita aliidhinisha mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya Daesh kaskazini-magharibi mwa Nigeria, akidai kundi hilo limekuwa likiwalenga Wakristo.

Marekani pia imeiwekea Afrika Kusini ushuru mkubwa wa kibiashara kutokana na madai ya “mauaji ya wazungu” — ambayo hayana msingi yanayodai kuwa kuna kampeni nchini humo ya kuwaua wakulima wazungu na kuwanyang’anya ardhi yao.

“Taifa linatakiwa kulaani na kukemea kilichotokea (Venezuela) kama ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Ni muhimu kufanya hivyo ili kuepusha kuwepo kwa mfano mbaya na kufikisha ujumbe kwa Trump, na pia kwa nchi nyingine, kwamba tabia kama hiyo haikubaliki na haitavumiliwa na dunia,” alisema Yusra Suedi, mhadhiri wa Sheria za Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Manchester, alipozungumza na TRT Afrika.

Wataalamu wanaeleza kuwa sheria za kimataifa haziruhusu taifa kumkamata kiongozi wa nchi huru isipokuwa kwa kujilinda au kwa idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

“Venezuela haikushambulia Marekani, wala haikuwa inapanga kuishambulia. Kwa kweli, Maduro alikuwa amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na Trump kuhusu biashara ya dawa za kulevya. Pia hakukuwa na idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hivyo ni wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria,” Suedi alieleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *