Akizungumza na waandishi wa habari kwa takriban dakika 30 ndani ya ndege ya Air Force One,Trump alizitaja Colombia, Cuba, Greenland, Mexico na Iran. Rais huyo wa Marekani amesema anatekeleza haki ya nchi yake kufanya itakavyo katika “maeneo yanayopakana na Marekani”.
Katika siku zilizofuata baada ya operesheni ya Venezuela, Trump ameongeza msisitizo juu ya nia yake ya kuitwaa Greenland kutoka Denmark. Asli Aydintasbas, mtafiti katika Kituo kinachohusika na masuala ya Marekani na Ulaya cha Taasisi ya Brookings, aliiambia AFP nikimnukuu, “Trump ametupa orodha ndefu ya maeneo yanayoweza kuwa malengo ya siku zijazo — lakini lengo linalowezekana zaidi kwa utawala wake litakuwa Greenland,”mwisho wa kumnukuu.
Trump anasisitiza kuwa Washington inahitaji eneo hilo lenye rasilimali nyingi za madini, ambalo lina mamlaka ya kujitawala kwa kiasi, kwa sababu za usalama wa taifa, akidai Denmark haina uwezo wa kuilinda Greenland dhidi ya Urusi na China.
Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, amejibu kwa kuonya kuwa jaribio lolote la kuitwaa Greenland kwa nguvu linaweza kumaanisha mwisho wa muungano wa kijeshi wa NATO unaoongozwa na Marekani.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema Washington inaweza badala yake kuongeza shinikizo la kidiplomasia kwa washirika wake wa Ulaya ambao tayari wana wasiwasi, kwa mfano kwa kusisitiza kufanyika kwa kura ya maoni Greenland.
Colombia pia imekuwa shabaha ya vitisho vikali zaidi vya Trump. Trump anamshutumu Rais Gustavo Petro kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya — kama alivyomshutumu Maduro kabla ya kukamatwa kwake. Petro, ambaye amekuwa akibadilishana maneno makali na Trump kwa miezi kadhaa kuhusu kampeni ya shinikizo la Marekani dhidi ya Venezuela, alijibu Jumatatu akisema alikuwa tayari “kuchukua silaha” kukabiliana na vitisho vya Trump.
Hata hivyo, Colombia inaweza kuleta changamoto ya aina tofauti kabisa, kutokana na kuwepo kwa makundi mengi yenye silaha yaliyosalia baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Badala yake, Trump huenda anaitumia Venezuela kuwaonya viongozi wengine wa Amerika ya Kusini watii masharti. Aydintasbas anasema, ‘anaweza kuitisha nchi ikubali kwa nguvu,’ na kwamba utawala wa Marekani lazima ukubalike iwapo wanataka kudumisha mamlaka yao.”
Trump alidai Jumapili kuwa Cuba — adui wa muda mrefu wa Marekani na mshirika wa Venezuela— ilikuwa “karibu kuanguka.” Cuba ilisema walinzi 32 wa Cuba waliuawa katika operesheni ya kumkamata Maduro. Lakini Trump alisema anaamini kuwa hatua za kijeshi dhidi ya Cuba hazitakuwa za lazima, akitabiri kuwa taifa hilo lililodhoofishwa na vikwazo haliwezi kustahimili kupoteza mafuta ya Venezuela yanayouzwa kwa ruzuku kubwa.
Jumapili hiyo hiyo, Trump aliambia Mexico kuwa inapaswa “kujipanga upya,” kufuatia miezi ya shinikizo kuhusu dawa za kulevya na biashara katika mpaka wa kusini wa Marekani.
Alisema Rais Claudia Sheinbaum wa Mexico ni “mtu mzuri sana,” na akaeleza kuwa anamsukuma kumruhusu kutuma wanajeshi wa Marekani kukabiliana na magenge ya dawa za kulevya nchini Mexico — pendekezo ambalo alisema Sheinbaum alikuwa amelilikataa awali. Sheinbaum alijibu Jumatatu kwa kupinga madai ya Marekani ya kutawala eneo hilo, akisema Amerika “si mali” ya mamlaka yoyote.
Iran — kama Venezuela ikiwa ni mzalishaji mkubwa wa mafuta — ilikumbwa na mashambulizi ya Marekani dhidi ya mpango wake wa nyuklia mwezi Juni na sasa iko chini ya shinikizo jipya kutoka kwa Trump kutokana na hatua zake kali dhidi ya waandamanaji.
Trump alionya Jumapili kuwa Tehran “itapigwa kwa nguvu sana” endapo waandamanaji zaidi watauawa.
Hata hivyo, Aydintasbas ameonya kuwa, “Kwa sasa Trump anaonekana kufurahia nafasi ya urais wa kifalme, lakini mambo yakianza kwenda kombo nchini Venezuela au Mashariki ya Kati, Trump atapoteza haraka sana hamu katika jukumu hili.”