Tume ya uchaguzi ya Uganda imeidhinisha vyama 27 kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa bunge na Urais, utakaofanyika Januari 15, kukiwa na wagombea urais wanane kwa ujumla wake wakiwemo rais wa sasa Yoweri Kaguta Museveni na kiongozi wa upinzani Robert Kyagulani anayefahamika zaidi kwa jina lake la usanii Bobi Wine.
Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 81anayeiongoza Uganda tangu mwaka 1986 anagombea muhula wa saba akiwa na chama chake kinachotawala cha National Resistance Movement NRM.
Waganda milioni 21.6 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu idadi hiyo ikiwa ni kubwa ikilinganishwa na ya uchaguzi uliopita wa mwaka 2021 ambapo tume iliandikisha wapiga kura milioni 18.1.
Katika idadi ya wapiga kura walioandikishwa na tume ya uchaguzi mwaka huu wanawake ni takriban asilimia 53. Licha ya ongezeko dogo la wapiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu, kimsingi wanaojitokeza siku ya upigaji kura kwa ujumla wake idadi yao imeonesha kuwa ndogo katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, kutoka kiasi asilimia 70 mnamo mwaka 2006 hadi chini ya asilimia 60 katika uchaguzi wa mwaka 2021.
Mfumo wa uchaguzi Uganda
Cha kutambuwa kuhusu namna uchaguzi unavyofanyika nchini humo, ni kwamba kwanza Uganda ina mfumo wa duru mbili za uchaguzi,ikiwa na maana kwamba mgombea wa urais anapaswa kupata ushindi wa zaidi ya asimilia 50 ili awe mshindi wa moja kwa moja ili kuepusha duru ya pili.
Na katika uchaguzi wa bunge wapiga kura watapaswa kuchaguwa wabunge 353 watakaowakilisha maeneo bunge ya nchi nzima, ingawa kuna viti maalum vya bunge ambavyo hutengwa kwa nafasi za wawakilishi wanawake, vijana na wenye ulemavu, wazee wafanyakazi na nafasi kwaajili ya wawakilishi wajeshi la UPDF pamoja na maafisa wa zamani.
Je, maafisa wa zamani hasa ni kina nani? Hawa ni wanachama wa zamani waliokuwa na vyeo ikiwemo makanu wa rais na waliokuwa mawaziri.Na hutengewa nafasi maalum endapo watashindwa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi kuingia bungeni.
Hata hivyo maafisa hao wa zamani huwa hawana haki ya kupiga kura katika masuala ambayo yanahitaji kupigiwa kura bungeni. Bunge la Uganda mnamo mwaka 2025 lilikuwa na viti 556 likiwa ni bunge kubwa zaidi barani Afrika lakini pia katika kanda hiyo ikilinganishwa na nchi kama Kenya,Ghana, Nigeria na Afrika Kusini.
Khofu ya uchaguzi kutokuwa huru
Katika uchaguzi huu wapiga kura hasa wana wasiwasi kuhusu ikiwa uchaguzi huo utakuwa wa uwazi na wa haki hasa hasa wakigusia mashaka yao juu ya uhuru wa tume ya uchaguzi, uwazi wakati wa kuhesabu kura na kwa ujumla ikiwa kweli kuna mazingira ya kuaminika kwa mchakato wenyewe.
Kuna khofu ya kutokea vurugu,watu kukamatwa na vitisho hasa dhidi ya wanasiasa wa upinzani na wafuasi wao na yote haya yanaibuwa wasiwasi kuhusu usalama,uhuru wa kiraia na usawa katika ushindani wa kisiasa.
Mpaka sasa mwanasiasa mkongwe wa upinzani Kizza Besigye amekuwa akishikiliwa jela akikabiliwa na kesi ya uhaini tangu Novemba 2024 baada ya kutekwa nyara Nairobi Kenya na kurudishwa Uganda.
Suala zima la ukosefu wa ajira, ughali wa maisha na fursa chache za kiuchumi hasa miongoni mwa vijana limebakia kuwa suala kubwa linalowashughulisha wapiga kura.
Lakini yote hayo yakitengeneza mazingira ya hali halisi kuelekea uchaguzi wa Januari 15,suala la wanasiasa kununua kura, kugawa rushwa na kuweko kwa sheria dhaifu za kudhibiti matumizi ya fedha kwenye kampieni nchini humo, huenda yakachangia kurubuniwa kwa wapiga kura na kutowa nafasi kwa wanasiasa wenye fedha kuibuka washindi.
