Mkutano huo utahudhuriwa na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Johann Wadephul, mwenzake wa Ufaransa Jean-Noël Barrot na Radoslaw Sikorski wa Poland. Hapo jana (06.01.2026), washirika wa Ukraine walikutana mjini Paris kujadili namna ya kuimarisha amani ya Ukraine kufuatia uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita. Changamoto katika kanda ya Indo pasifiki pia ni jambo litakalojadiliwa katika mkutano huo.
Waziri wa mambo ya nje wa India Subrahmanyam Jaishankar anatarajiwa kujiunga na muungano huo wa pande tatu wa Wiemar unaozijumuisha Ujerumani, Ufaransa, na Poland kujadili namna ya kuimarisha uhusiano kati ya Ulaya na India. Kundi la Weimar liliundwa mwaka 1991 nchini Ujerumani katika mji ulio na jina hilo la Weimar.
Jana Jumaane (06.01.2026), viongozi wa Ufaransa Uingereza na Ukraine walitia saini makubaliano yanayokusudiwa kupelekea kikosi kinachojumuisha nchi tofauti za Ulaya Ukraine kama sehemu ya hakikisho la usalama kwa nchi hiyo baada ya makubaliano ya usitishaji vita kufikiwa. Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema Ujerumani huenda ikajumuishwa pia katika kikosi hicho.
Katika utiaji saini huo, Waziri Mkuu wa Uingereza Kier Starmer alisema makubaliano hayo yanaonesha moja kwa moja nia ya mataifa hayo ya kusimama na Ukraine kwa muda mrefu. Starmer alisema baada ya makubaliano ya usitishaji vita kufikiwa Uingereza na Ufaransa zitaweka maeneo ya kijeshi Ukraine na kujenga maeneo ya ulinzi ya kuhifadhi silaha ili kuiwezesha Ukraine kuendelea kujilinda. Rais Zelensky amepongeza maafikiano hayo.
Mazungumzo ya Kiev na Washington kuendelea
Kwengineko maafisa wa Marekani na Ukraine wataendelea leo na mazungumzo yao kuhusu uhakikisho wa usalama wa Kiev. Baada ya mkutano mkubwa wa muungano wa washirika wa Ukraine mjini Paris, wajumbe wote wa Marekani na Ukraine wametoa matumaini ya muelekeo mzuri katika mazungumzo yao.
Rais wa Ukraine Volodymr Zelebsky na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff wametoa hakikisho hilo la mazungumzo kuendelea leo Jumatano. Zelensky aliishukuru Marekani kwa kuonyesha nia ya kuiunga mkono kikamilifu.
“Nataka kumshukuru kila kiongozi, nataka kuishukuru kila nchi inayotaka kweli kuwa ssehemu ya mpango huu wa amani. Tumezungumza kwa kwa kirefu leo na timu ya Marekani kuhusu ufuatiliaji ili kuzuia ukiukwaji wa amani. Marekani iko tayari kufanya kazi katika hili. Hili ni muhimu sana kwetu,” alisema Zelensky.
Hata hivyo Marekani imetahadharisha kwamna hakikisho la usalama kwa Ukraine litakuja baada ya makubaliano ya usitishaji vita vya takriban miaka minne kufikiwa. Hata hivyo nia ya rais wa Urusi Vladimir Putin katika hili bado haijajulikana.
