Mpango wa ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo tatu, pamoja na mipango miwili ya ushirikiano kati ya Jeshi la Israel, IDF na Vikosi vya Ulinzi vya Ugiriki, na kati ya IDF na Jeshi la Cyprus, ulisainiwa nchini Cyprus wiki iliyopita. Makubaliano hayo yalisainiwa mjini Nicosia wakati wa mkutano wa kila mwaka wa wakuu wa majeshi wa nchi hizo tatu na ulitangazwa rasmi na IDF, na kupata mwitikio mzuri kutoka kwenye vyombo vya habari vya ndani na umma wa Cyprus.

Ingawa taarifa zaidi za makubaliano hazijawekwa wazi, DW imegundua kuwa yanajumuisha vipengele vya mazoezi na mafunzo ya pamoja, uanzishwaji wa vikosi vyenye ujuzi katika maeneo maalum na maendeleo ya mazungumzo ya kimkakati ya kijeshi. Kulingana na duru hizo hizo, makubaliano hayo yanatoa pia fursa ya kubadilishana ujuzi na utaalamu kuhusu vitisho vya kisasa vya usalama, kama vile mifumo ya droni na mifumo ya vita vya kielektroniki.

Israel Jerusalem 2025 | Mkutano wa nchi tatu kati ya Israel, Ugiriki na Cyprus
Viongozi wakuu wa Israel, Ugiriki na CyprusPicha: Abir Sultan/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Tangazo hilo la ushirikiano wa kijeshi linatekeleza vyema uamuzi wa kisiasa uliochukuliwa na viongozi wa nchi hizo tatu: Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Rais wa Cyprus, Nikos Christodoulides, pamoja na Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis, wakati wa Mkutano wa Kilele wa 10 wa pande hizo tatu mnamo Desemba 22, mwaka 2025.

Akitoa muhtasari wa taarifa yao ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano wa Jerusalem, Rais Christodoulides alisema kwa wakati huo nchi hizo tatu ziliamua kuimarisha ushirikiano wao, kwa kuangazia nishati, ulinzi na usalama, akirejelea makubaliano ambayo yatahamia mara moja kwenye hatua ya utekelezaji.

Akizungumza na DW, Zenonas Tziarras, mhadhiri katika Idara ya Mafunzo ya Kituruki na Mashariki ya Kati kwenye Chuo Kikuu cha Cyprus, alibainisha kuwa ushirikiano kati ya nchi hizo tatu, sio mpya, na kwamba mkutano wa kwanza wa kilele wa aina hiyo ulifanyika mwaka 2016.

Akisisitiza kwamba Ugiriki, Cyprus na Israel zimekuwa zikishirikiana katika nyanja hizo kwa miaka mingi, Tziarras amesisitiza kwamba licha ya tabia ya muda mrefu ya viongozi wa kisiasa ya kuzidisha matokeo ya mkitano hiyo, inapaswa kuwa wazi kwamba ”ushirikiano wa kijeshi, ulinzi na usalama wenyewe haujengi muungano.”

Kimsingi Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan tofauti na vyombo vya habari vya Uturuki vinavyoiunga mkono serikali kuuelezea ushirikiano huo kama ”mhimili wa uovu dhidi ya Uturuki”, vilikuwa na msimamo wa wastani, vikisema kwamba mipango ya nchi hizo tatu, ”haina uzito wowote,” yaani sawa na debe tupu ” halikosi kelele.”

Zypern Nikosia 2023 | Netanyahu na Mitsotakis
Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis (kulia) alipokutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya rais katika mji mkuu wa Cyprus Nicosia mnamo Septemba 4, 2023.Picha: Petros Karadjias/AFP

Kinachoonekana kuipa wasiwasi Uturuki zaidi ya makubaliano ya pande tatu yenyewe, ukweli ni kwamba Ugiriki na Cyprus zinazidi kuigeukia Israel kwa ajili ya manunuzi ya mifumo ya silaha za juu. Kwa upande wake, Cyprus imetoa onyo kali kwamba manunuzi ya silaha kutoka Israel yanaweza kusababisha msukosuko katika kisiwa hicho.

Mwezi Septemba, 2025 Uturuki ilikosoa vikali sana wakati mfumo wa ulinzi wa anga wa Barak MX uliotengenezwa na Israel ulipowekwa na kuanza kufanya kazi nchini Cyprus. Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilielezea kupelekwa kwa mfumo huo kama kitisho kwa utulivu wa kikanda. Ilionya kwamba sera za upande wa Cyprus zinadhoofisha utulivu na amani katika eneo hilo na zinahatarisha kuchochea kuonyeshana nguvu za silaha kisiwani humo.

Hata hivyo, uwekaji wa mfumo huo bado haujakamilika kutokana na vita vya Gaza, ingawa maafisa wa jeshi la Cyprus tayari wamepewa mafunzo nchini Israel kwa ajili ya uendeshaji wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *