Katika ripoti mpya iliyotolewa Jumatano na iliyokosolewa na Israel, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imekemea vitendo vya ubaguzi dhidi ya Wapalestina katika maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kimabavu na kusisitiza kuwa hali “imezidi kuwa mbaya” katika miaka ya hivi karibuni.
Mkuu wa Ofisi hiyo ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa Volker Turk amesema kumekuwepo kwa miongo kadhaa sasa “ubaguzi wa kimfumo” dhidi ya Wapalestina na kwamba hilo limekuwa tatizo la muda mrefu, akisisitiza kuwa hali imezorota mno kuanzia Desemba mwaka 2022.
Turk ameongeza kuwa mamlaka za Israel zimekuwa na undumilakuwili kwenye sheria na sera zake huku kukiwa na utofauti wa namna wanavyoshughulikiwa walowezi wa Israel na Wapalestina wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi, na hivyo kusababisha hatua zisizo na usawa katika masuala mbalimbali muhimu ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa ardhi na kuwazuia katika ufikiaji wa rasilimali.
Turk ameendelea kuwa uminywaji wa kimfumo wa haki za Wapalestina unaendelea katika Ukingo wa Magharibi , iwe katika upatikanaji wa maji, kwenda shule, kupata matibabu hospitalini, kutembelea familia au marafiki, au hata kuvuna mizeituni, na kwamba karibu kila nyanja ya maisha ya Wapalestina inadhibitiwa na kuzuiwa na sheria, sera na vitendo vya kibaguzi vya Israel. Amesema hatua hizi zinakiuka sheria za kimataifa zinazozitaka nchi kupiga marufuku na kutokomeza ubaguzi wa rangi na mifumo ya ubaguzi wa kudumu.
” Hali zote mbaya zilizobainishwa katika ripoti hii si tu zinaendelea, bali pia zimezidi kuongezeka,” amesisitiza Turk.
UN yatoa tahadhari kuhusu kuzorota kwa hali
Mkuu huyo wa Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa Volker Turk ametahadharisha kuwa kuruhusu kuendelea kwa hali hiyo kunapelekea matokeo yake kuzidi kuwa mabaya kwa Wapalestina, huku akizitaka mamlaka za Israel kuachana kabisa na sheria, sera na desturi zote kandamizi dhidi ya Wapalestina, ubaguzi aliosema unafanywa kwa kuzingatia misingi ya rangi, dini au asili.
Aidha, Turk ametoa wito kwa Israel kuheshimu haki ya watu wa Palestina ya kujiamulia mambo yao wenyewe huku akiitaka pia kusitisha uwepo wake kinyume cha sheria katika eneo la Wapalestina linalokaliwa kimabavu, ikiwa ni pamoja na kubomoa makazi yote na kuwaondoa walowezi.
Hii ni mara ya kwanza kwa mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kusema wazi kuwa vitendo vya Israel dhidi ya Wapalestina ni aina ya mfumo wa “ubaguzi wa rangi” ama “Apartheid” ambao uliwahi kushuhudiwa katika nchi kama Afrika Kusini.
Ujumbe wa kidiplomasia wa Israel katika Umoja wa Mataifa huko mjini Geneva umekosoa vikali “shutuma hizo na kuzitaja kuwa za kipuuzi, za upotoshaji na zenye lengo la kuifachua Israel”.