Upatanishi ni jukumu la wote kukuza umoja wa kitaifaUpatanishi ni jukumu la wote kukuza umoja wa kitaifa

KATIKA dunia ya leo ambako utawala bora unaendelea kuimarika, uchaguzi mkuu katika mfumo wa siasa wa vyama vingi ni msingi wa maisha ya kidemokrasia.

Mazingira hayo ya uchaguzi ndiyo huwezesha raia kuchagua viongozi, kujadili hoja na kuweka mwelekeo wa hatima ya taifa. Hata hivyo, kama historia inavyoonesha, uchaguzi unaofanyika katika mazingira hayo hasa ya ushindani mkali, mara nyingi huacha hisia kali za kisiasa na migawanyiko ya kijamii.

Katika mazingira ya aina hiyo, madai ya ukiukwaji wa taratibu, kutoaminika kwa taasisi, kauli za kisiasa za uchochezi na simulizi za ‘kutia chumvi’ za vyombo vya habari ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuvuruga jamii baada ya kura kuhesabiwa.

Baada ya uchaguzi katika mfumo huo wa siasa, huku viongozi wakiwa wamechaguliwa, suala la upatanishi na kuponya jamii si la hiari; bali la msingi kwa ustawi (uimara) wa kijamii, kufufua uchumi na kuunganisha demokrasia.

Jambo muhimu zaidi katika kupata upatanishi wenye maana, ni suala la kuhusisha jamii. Wakati viongozi na taasisi za kitaifa wakiwa na jukumu kubwa katika hili, uponyaji wa kweli unaanzia ngazi ya chini yaani katika vijiji, kwa majirani, katika sehemu za kazi, taasisi za kiimani na hata katika majukwaa ya kiraia wanakoishi raia na athari za mgawanyiko wa kisiasa.

Katika chaguzi nyingi za vyama vingi, mchakato wa kuchagua viongozi mara nyingi unahusisha makundi mbalimbali yanayounga mkono wagombea tofauti nchi nzima. Hata hivyo, baada ya uchaguzi na baada ya wagombea wanaoshindana kuchaguliwa, taifa lazima litambue hitaji la kukabiliana na migawanyiko hii na kuungana ili kukuza maendeleo ya taifa.

Hakuna ubishi kuwa, uchaguzi wa vyama vingi hutoa washindi na washindwa. Ushindani wa kisiasa unapokuwa mkali, matokeo ya uchaguzi yanaweza kuibua hisia za kutengwa, kutotendewa haki, au hofu miongoni mwa watu. Jamii au watu binafsi wanaweza kugawanyika kwa misingi ya vyama, ukoo, ukanda, dini au hata vizazi.

Hali inapokuwa mbaya zaidi, uchaguzi unaweza kuzaa maandamano, vurugu, kauli za chuki, migomo ya kiuchumi au kutoaminiana kwa muda mrefu katika jamii. Historia katika nchi nyingi za kidemokrasia inaonesha kuwa, malalamiko baada ya uchaguzi ambayo hayapatiwi ufumbuzi mapema, hudhoofisha uhalali wa dola, huzorotesha uwekezaji, hufifisha shughuli za kiuchumi na huondoa mshikamano wa kijamii.

Katika mazingira hayo, biashara huchelewa kupanuka, jamii hupoteza imani kwa taasisi za ndani na hata raia wanakuwa katika hatari ya kujiweka kando katika juhudi za maendeleo ya taifa. Bila ya upatanishi, mzunguko wa kisiasa unakuwa muundo wa hofu unaojirudia badala ya maendeleo.

Hivyo, upatanishi wa kitaifa haupaswi kuchukuliwa kama kaulimbiu ya kisiasa au tukio la mara moja, la hasha. Kwangu mimi, upatanishi ni mchakato endelevu wa kujenga tena imani, kurudisha utu na kuthibitisha tena misingi ya taifa.

La muhimu na msingi zaidi ni kuwa, upatanishi si suala la kulazimisha watu kusahau malalamiko yao au kunyamazisha hoja zenye ‘mashiko’, ni kutengeneza nafasi safi na salama ya watu ‘kutema nyongo’ zao kwa amani na kwa hoja za kujenga, sambamba na kuwa na muda wa kuibua na kujifunza yale ambayo pengine hayakusimamiwa vizuri.

Ndio maana serikali, vyama vya upinzani, taasisi za kijamii, viongozi wa kimila, taasisi za kidini, vyombo vya habari na raia wote wana jukumu la kutimiza katika kuhakikisha umoja na amani ni silaha na nyenzo muhimu kwa ustawi wa taifa. Kwa kujifunza kutoka kwa wengine, ni wazi upatanishi unaohusisha majadiliano ya ‘vigogo’ wa kisiasa mara nyingi hukwama na haufikii mahitaji halisi ya kila siku ya raia.

Ndio maana kwa maoni yangu, ushirikishwaji wa jamii si tu kwamba ni jambo muhimu, bali pia lisilokwepeka. Kimsingi, kuhusisha jamii kuna maana ya kuhusisha kikamilifu raia katika majadiliano, uamuzi, kutatua matatizo na kuchukua hatua kwa pamoja.

Baada ya uchaguzi, kuhusisha jamii husaidia kubadili ushindani wa kisiasa kuwa ushirikiano wa kijamii na hubadili tofauti za kisiasa kwa kukumbusha raia kwamba majirani, rafiki na familia wana mengi ya kushirikiana kuliko yanayowagawa.

Kwa mfano, katika jamii ambazo mivutano imekuwa mikubwa baada ya uchaguzi, majukwaa ya sehemu husika yanayosimamiwa na viongozi wa kijamii yanawezesha raia kueleza machungu yao, kufafanua upotoshaji na kusikiliza mawazo mbadala.

Majukwaa kama hayo yanapunguza uvumi na kuzuia kuendelea kwa mgogoro kwa kutatua masuala mapema na kwa uwazi, na hapo, jukumu la viongozi wa imani ni muhimu. Viongozi wa dini na wale wa kitamaduni mara nyingi wanaaminika kimaadili, jambo ambalo ni zaidi ya kuwa mfuasi wa chama.

Kuhusika kwao katika mchakato wa upatanishi kwa kupitia maoni, hujenga uaminifu na imani. Katika jamii nyingi, viongozi hawa wanaweza kuitisha majadiliano baina ya vyama au baina ya jamii ambayo wanasiasa wanaweza kupata ugumu kuyafanikisha bila kutiliwa shaka.

Kwa mfano, taasisi za imani zinaweza kuitisha sala za pamoja, mahubiri ya amani na shughuli za huduma za kijamii zinazowaleta pamoja wafuasi wa vyama tofauti vya siasa. Kubadilishana misingi ya kiroho na kimaadili pia kunasaidia kubadili mitazamo ya kutokukubaliana kisiasa kwa muktadha mkubwa wa umoja, huruma na uwajibikaji kwa taifa.

Pamoja na viongozi wa dini, vijana mara nyingi ndio huwa katikati ya mivutano baada ya uchaguzi, ama kama wahamasishaji wa kisiasa, au waathirika wa hila za kisiasa. Wakati huo huo, vijana wanawakilisha fursa kubwa zaidi ya upatanishi endelevu.

Kuwashirikisha vijana katika shughuli kama michezo, sanaa, programu za ujasiriamali na mipango ya elimu ya uraia kunaweza kubadili nguvu zao za kisiasa na kutumika kwa manufaa kujenga taifa. Kwa mfano, majadiliano yanayoongozwa na vijana yanaweza kusaidia kutatua masuala ya ukosefu wa ajira, kutumika kisiasa na upotoshaji au upotoshwaji kidijiti.

Vijana wanapopewa majukwaa ya kujadili shida zao na kuchangia majawabu, wanakuwa mabalozi wa amani kuliko kuwa mawakala wa mgawanyiko au makundi ya watu wanaoibua vurugu bila kujua athari za uamuzi wanaofanya kwa ajili yao na taifa kwa ujumla.

Katika kusaka amani na mshikamano wa kudumu, nafasi na jukumu la wanawake au mama wanaokuza na ambao ni walimu wetu wa kwanza, ni muhimu. Kimsingi, wanawake wana mchango mkubwa katika jukumu la upatanishi. Kama walezi na wachangiaji muhimu katika uchumi, wanawake ni waathirika wakubwa wa kukosekana kwa utulivu baada ya uchaguzi.

Si siri, mipango ya kuhusisha jamii inayowezesha wanawake kupitia makundi ya kujiwekea akiba na kamati za amani na juhudi za usuluhushi, huimarisha ustahimilivu wa kijamii. Vyombo vya habari navyo vina jukumu kubwa kuchagiza simulizi za baada ya uchaguzi.

Uandishi wa habari wa uwajibikaji husaidia na kuchochea upatanishi kwa kusisitiza ukweli, kupaza sauti za umoja na kukataa kauli za uchochezi. Redio za kijamii zinaweza kutumika kama majukwaa ya majadiliano, kufikisha ujumbe wa amani na elimu ya uraia.

Kuhusisha jamii na vyombo vya habari kupitia programu za kupiga simu na matangazo ya kwenye kumbi, kunasaidia kukabili upotoshaji na kurejesha imani. Raia wanaposikiliza maoni yao yakiwasilishwa kwa heshima katika vyombo vya habari, wanajisikia kuhusishwa katika majadiliano ya kujenga taifa.

Hali ngumu za uchumi wakati mwingine huchangia migawanyiko ya kisiasa. Mipango ya kijamii ya uwezeshaji kiuchumi kama ushirika, masoko ya pamoja, miradi ya miundombinu au kamati za maendeleo katika maeneo husika inaweza kusaidia upatanisho kwa kukutanisha mahasimu wa kisiasa katika jambo lenye maslahi ya pamoja kiuchumi.

Kwa mfano, wakulima kutoka vyama tofauti vya siasa wanaofanya kazi katika ushirika, wanaweza kuweka kipaumbele katika uzalishaji badala ya uadui wa kisiasa. Malengo yanayofanana ya kiuchumi pia husaida kubadili uhusiano mbaya kuwa ubia na hivyo, kudumisha amani kupitia ushirikiano wa vitendo.

Kimsingi, upatanishi wa kitaifa si tu jambo juu ya kuvumilia tofauti, bali pia kujenga ushirikiano wa maana wenye kusudi la kuleta maendeleo na kujenga umoja wa kitaifa. Aidha, ushirikishwaji jamii hushawishi raia kuona uchaguzi kama sura moja katika simulizi ndefu ya taifa kuliko shindano moja lililowekwa pamoja.

Inawakumbusha watu kuwa demokrasia si tu inamea wakati upande mmoja ukitawala lakini pia jamii inapobaki kitu kimoja, hata kama kuna kutokukubaliana. Hili ni muhimu kwa sababu uponyaji unachukua muda. Unahitaji subira, unyenyekevu na uongozi bora katika pande na ngazi zote.

Muhimu zaidi, upatanishi unapaswa kuwa makini na wala si utendaji. Upatanishi hauna budi kuwa uliojengwa katika elimu ya uraia, utawala wa wananchi wenyewe na mikakati ya maendeleo ya taifa, muda mrefu kabla ya uchaguzi mwingine.

Baada ya uchaguzi mkuu wa vyama vingi, mtihani wa kweli wa demokrasia unajikita si tu katika kuaminika kwa kura, bali pia katika uwezo wa taifa kupona na kwenda mbele pamoja. Upatanishi wa taifa na kuponya kupitia kuhusisha jamii hutoa njia endelevu ya amani, utulivu na maendeleo ya pamoja.

Jamii inapozungumza na kufanya kazi kwa pamoja sambamba na kusikiliza kwa huruma, vidonda vya kisiasa vinaweza kupona. Uchaguzi unaweza kuwa na maoni kinzani lakini hayapaswi kuligawa taifa, kiasi cha kushindwa
kulijenga upya.

Kupitia majadiliano ya makusudi ya pamoja, jamii zinaweza kubadili mivutano ya baada ya uchaguzi kuwa fursa za kujenga upya umoja na kushirikiana katika maendeleo ya taifa. Kimsingi, Watanzania hawana budi kukumbuka kuwa upatanishi si jukumu la viongozi pekee, bali pia ni jukumu la pamoja la raia wanajitolea kwa ajili ya hatima ya nchi yao yenye umoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *